TIMU ya U-23 ya Tanzania imeshindwa kuwatambia vijana wenzao wa Nigeria baada ya kukubali kufungwa mabao 3-0 katika mechi ya marudiano kwenye uwanja wa Samuel Ogbemudia mjini Benin hivyo kutolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania kucheza michezo ya Olimpiki 2012 mjini London.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam vijana wa Tanzania walishinda bao 1-0 hivyo kutolewa kwa mabao 3-1 na Nigeria.
Vijana wa Tanzania walitakiwa kushinda au kutoa sare ya aina yoyote ili waingie hatua ya makundi ambayo itashirikisha timu nane na baada ya hapo ni timu tatu ndio zitakazofuzu kucheza olimpiki hata hivyo vijana wa Nigeria walikuwa imara.
Dakika za mwishoni za mchezo vijana wa Nigeria walionekana kuchoka ambapo vijana wa Tanzania walipeleka mashambulizi kwenye lango la Nigeria wakiamini wakipata bao moja watakuwa wameitoa Nigeria, lakini bahati haikuwa yao.
Timu hizo zilienda mapumziko huku Nigeria ikiongoza kwa bao 1-0, bao ambalo lilifungwa na Ekigho Ehiosun katika dakika ya tano baada ya kuunganisha krosi ya Lukman Haruna aliyekuwa akijitahidi sana uwanjani kwenye winga ya kulia.
Lakini katika kipindi hicho cha kwanza dakika ya 12 kipa wa vijana wa Tanzania, Seif Juma aliumia na nafasi yake ilichukuliwa na Jackson William.
Vijana wa Tanzania walionekana kuelemewa katika dakika 20 za mwanzo wa mchezo, lakini baadaye walibadilika huku Thomas Ulimwengu akifanya vizuri katika safu ya ushambuliaji.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kushambuliana, lakini walikuwa wanigeria ambao walipata bao la pili lililofungwa na Ganiyu Oseni katika dakika ya 56 baada ya kupata pasi kutoka winga ya kulia iliyotolewa na Ekigho Ehiosun.
Baada ya Nigeria kupata bao hilo la pili alionekana aliyekuwa mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Nigeria, Kanu “Papillo” Nwankwo akiungana na makocha wa Nigeria kuwaelekeza wachezaji wa Nigeria.
Kocha wa Vijana wa Tanzania, Jamhuri Kihwelu aliamua kumtoa Abuu Ubwa katika dakika ya 64 na nafasi yake kuchukuliwa na Issa Rashid na ilipofika dakika ya 70 vijana wa Tanzania walibadilika tena kimchezo na kuanza kupeleka mashambulizi katika lango la Nigeria.
Nigeria ilipata bao la tatu katika dakika ya 90 lililofungwa na Ahmed Musa baada ya kupata pasi kutoka kwa Ekigho Ehiosun ambaye aliwatoka mabeki wa vijana wa Tanzania na kutoa pasi iliyomkuta mfungaji akiwa peke yake.
Mechi ya timu ya Vijana ya Tanzania dhidi ya Nigeria ilitakiwa ichezwe juzi, lakini uwanja huo ulijaa maji ndipo kamishana wa mechi hiyo Emmanuel Zombre kutoka Burkina Faso alipoamua pambano hilo liahirishwe baada ya kusubiri kwa muda wa saa moja.
Mvua hiyo kubwa ambayo iliijaza maji sehemu ya kuchezea ilianza kunyesha wakati vijana wa Tanzania na wale wa Nigeria walikuwa wakifanya mazoezi ya viungo uwanjani.
Wakati huo huo; Timu za vijana za Afrika Magharibi na Kaskazini zimeendelea kutamba kwenye michuano hiyo baada ya Algeria, Morocco, Ivory Coast, Misri na Senegal kufuzu kwa hatua ya makundi.
Algeria imefuzu kwa hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 pamoja na Jumamosi kufungwa 0-2 na Zambia mjini Chingola.
Mabao ya Zambia yalifungwa na Venicious Mapanda na Derrick Mwanza, lakini hayakutosha kuwasogeza mbele baada ya mchezo wao wa kwanza kuchapwa 3-0.
Jijini Cairo, wenyeji Misri walikata tiketi ya makundi kwa ulaini baada ya kuichapa Sudan 2-0, mabao ya Misri yalifungwa katika kipindi cha pili na Ahmed Sherweda na Shehab Ahmed.
Nao Tembo watoto wa Ivory Coast walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Congo. Shangwe katika jijini Abidjan ziliamshwa na mshambuliaji wa ASEC Mimosas, Jean-Jacques Bougouhi aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 10 ya mchezo na kuwawezesha kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya mchezo wa kwanza jijini Brazzaville kumalizika 2-1.
Jijini Kinshasa, kiungo wa TP Mazembe, Deo Kanda alifunga bao la kuongoza kwa DR Congo, lakini Ahmed Allah wa Morocco alisawazisha bao hilo na kuilazimisha DR Congo kwenda sare ya 1-1 hivyo Morocco kusonga mbele kwa jumla 3-1 kwa sababu katika mechi ya kwanza ilishinda 2-1.
Mechi nyingine zilizotakiwa kuchezwa jana zilikuwa ni kati ya Mali dhidi ya Gabon huko mjini Bamako na Afrika Kusini dhidi ya Benin mjini Johannesburg.
Simba waangukia pua
Kinshasa
NDOTO ya Simba kucheza Kombe la Shirikisho msimu huu ilifutika rasmi jana baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Daring Club Motema Pembe kwenye Uwanja wa Kamanyola jijini Kinshasa.
Simba iliyopata nafasi ya kucheza michuano hiyo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya TP Mazembe na kufanikiwa kucheza mechi moja na Wydad Casablanca ili kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa lakini vigogo hao wa Tanzania walipoteza kwa kuchapwa 3-0.Hivyo ikapata nafasi ya kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya DC Motema Pembe ili ipata tiketi ya nane bora.
Simba watajutia nafasi saba walizopata na kushindwa kuzitumia kupita washambuliaji wake Musa Mgosi, Emmanuel Okwi na Shija Mkina katika kipindi chote cha kwanza.
Mshambuliaji wa DC Motema Pembe, Lamana Bokoto aliwafundisha wakina Mgosi namna ya kutumia nafasi kwa kufunga bao la kuongoza kwa Wacongo hao dakika 37, akiunganisha krosi kwa kichwa iliyoganga mwamba na kudunda chini na kipa Juma Kaseja alijaribu kuokoa, lakini mwamuzi akasema ni goli.
Uzembe wa mabeki wa Simba katika kuokoa mpira ulitoa mwanya kwa Tresor Salakyaku kufunga bao la pili kwa Daring dakika ya 66.
Baada ya mabao hayo wachezaji wa Motema walikuwa wakijiangusha kila dakika kwa lengo la kupoteza muda huku mashabiki wao wakishangilia na kuwasha mishumaa uwanja mzima.
Mashabiki wa Vilal waliokuwa waikishangilia Simba walipiga vitendo hivyo na kuanza kutupa vitu uwanjani na kuwafanya askari kuanza kuwakimbiza majukwaani watoke nje.
Simba walianza mchezo wao kwa kasi na kuonyesha kutulia zaidi kwenye nafasi ya kiungo huku washambauliaji wake Mussa Hassan Mgosi, Emmanuel Okwi wakiongoza mashambulizi kwa nguvu.
Shija Mkina alikosa bao la wazi baada ya Okwi kutengeneza pasi safi lakini shuti lake lilipaa juu, beki ya DC Motema Pembe ilipoteza ushirikiano na umakini tofauti na ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza.
Simba walipoteza nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Mohamed Banka ambaye shuti lake lilipaa dakika ya 25, kabla ya Mgosi kushindwa kufunga akiwa yeye na kipa dakika 31, kwa shuti lake kupanguliwa na kukosa maliziaji.
Uwanja wa Kamanyora huo ulijaa Askari wengi, lakini washindwa kuzuia vurugu za mashabiki waliojaa uwanjani hapo, huku mashabiki wa klabu ya Vital wakiwa waunga mkono Simba muda wote wa mchezo.
CHANZO, gazeti Mwananchi