Vijana Watakiwa Kufanya Kazi kwa Kutumia Fursa Zilizopo

Sehemu ya umati wa watu ukiwa kwenye Matembezi ya mshikamano ya kuitaka Serikali iendelee kuzilinda fursa zilizopo na pia kuendelea kuutanua wigo wa upatikanaji wa fursa hizo kwa wasanii na vijana wenyewe katika nafasi ya kujikwamua kimaisha,ikiwa sambamba na kupinga uwizi/uharamia wa kazi za sanaa hapa nchini, yaliyoanzia kwenye uwanja wa Jamhuri na kufikia tamati viwanja vya Nyerere Skwea.


 
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amehimiza vijana wa Tanzania kuwa na uthubutu wa kujaribu kuzifanyia kazi fursa zilizopo katika sekta tofauti kama vile ujasiriamali, kilimo, viwanda, sanaa na utamaduni ambazo zinapatikana kwenye maeneo wanayoishi.
 
Alisema kwa mujibu wa Sensa ya Makazi na Watu ya mwaka 2012, Tanzania ina idadi kubwa ya watu wenye uwezo wa kufanya wazi, wanaofikia asilimia 52 ya watu wote, na wengi wao ni vijana na asilimia 48 wanaobakia ni wazee na watoto. “Hivyo basi, nchi yetu inaweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kama kundi hili lote la vijana litaamua kutumia kikamilifu fursa zilizopo nchini za kujiletea maendeleo,” alisisitiza.
 
Alikuwa akizungumza na mamia ya vijana wa mji wa Dodoma na Dar es Salaam baada ya kupokea maandamano ya kutangaza kampeni ya kupenda na kutumia bidhaa na huduma za Tanzania maarufu kama “Made In Tanzania” yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere mjini Dodoma, Jumapili, Mei 12, 2013.
 
Kampeni hiyo ya Made in Tanzania inayoendeshwa na kampuni ya Clouds Media Group ilianza Machi, mwaka huu, kwa lengo la kutambua watu, bidhaa, mashirika, muziki na utamaduni wa Kitanzania na imelenga kutangaza bidhaa na huduma za Tanzania.
 
Alisema wako watu walianza ujasiriamali kwa kuuza karanga lakini walipanda hadi kuwa na biashara kubwa kwa sababu walitambua fursa zilizokuwepo na wakazifanyia kazi bayana. “Kikubwa ni kuwa na dhamira na malengo, lakini fursa ziko kwenye kilimo, viwanda, ufugaji nyuki, ufugaji kuku wa asili ama mapishi ya chakula,” aliongeza.
 
Alisema anafurahishwa na mwamko uliopo hivi sasa kwa baadhi ya vijana waliohitimu vyuo vikuu ambao wameamua kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha miradi yao. “Wako vijana waliohitimu ambao wameomba misaada Serikalini na wakaanzisha miradi huko waliko. Wengine wako Igunga, Iramba, Tarime, Rufiji na Mkuranga,” alifafanua.
 
Alisema wako walioamua kujihusisha na kilimo cha alizeti, na wengine wameamua kufuga kuku wa asili na kuamua kuwauza Dar es Salaam ambako walibaini kuna soko la uhakika kwa bei ya sh. 10,000/- hadi 15,000/- kwa kuku mmoja.
 
Alisema licha ya kudumisha mapenzi ya dhati na kujenga uzalendo kwa nchi na watu wake, kampeni hiyo pia inalenga kuonyesha ufahari wa yote yanayowazunguka Watanzania, ufahari ambao upo ndani ya kila mmoja.
 
“Made in Tanzania kwa ujumla wake ni kampeni ambayo mmeileta mahsusi kusaidia vijana kwa kuwahimiza kuona fursa za kiuchumi na za maendeleo zilizopo ambazo zikitumiwa vizuri zitawezesha vijana na Taifa kwa ujumla kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo”.
 
Alisema kwa vile kampuni ya Clouds Media Group imeamua kwemnda mikoa yote hapa nchini, haina budi kuvishirikisha vyombo vingine vya habari ili kampeni hiyo iweze kuwa pana zaidi na kupata mwitiko wa kitaifa.
 
Akizungumzia kuhusu kazi za wasanii hapa nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali italinda uhalali wa kazi za wasanii wa Tanzania na ndiyo maana ikaamua kuanzisha mfumo wa matumizi ya sticker za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
 
Mapema, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Bw. Rugemalira Mutahaba alisema kampuni yake kama chomcho cha habari wameamua kuendesha kampeni hiyo ili kuwaelekeza vijana wa Kitanzania fursa zipi zilizopo, wafanye nini ili kuzipata na zaidi ya yote kuwahimiza vijana hao wa wajifunze kuwa na uthubutu wa kutenda mambo bila woga.
 
Alisema kampuni yake ilialika vijana 150 kutoka Dar es Salaam ili wafike Dodoma kujumuika na vijana wenzao wa Dodoma ambao walishiriki semina maalum kuhusu fursa zilizopo nchini iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma na kushirikisha vijana zaidi ya 2,000.