Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya vijana wa kundi la 4U Movement waliokuwa wakimuunga mkono Edward Lowassa leo wamerudisha kadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza na mtandao huu mmoja wa wawakilishi wa vijana hao, Michael Litanda alisema takribani vijana 100 waliokuwa katika kundi hilo la 4u Movement wameamua kukihama Chama Cha Mapinduzi ikiwa ni kutoridhishwa na kitendo alichofanyiwa mfuasi wao Edward Lowassa kwenye mchucho wa wagombea nafasi ya urais kupitia CCM uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.
Alisema katika kundi hilo baadhi ya vijana ni wanafunzi wa vyuo vikuu na vijana wengine wanaofanya shughuli mbalimbali jijini Dar es Salaam na walikuwa wakimuunga mkono Lowassa. Wakifafanua zaidi baadhi ya vijana waliojitokeza leo eneo la Mwananyamala baadhi ya vijana hao walisema si vijana wote ambao wamepata nafasi ya kukusanyika kutokana na shughuli mbalimbali lakini wapo takribani vijana 100 ambao wameamua kukihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na Chadema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Jimboa la Kinondoni jijini Dar es Salaam, Waziri Muhuzi akiwapokea vijana hao alisema anawakaribisha vijana hao kwa kuhamia chama sahihi cha Chadema na milango ipo wazi. Alisema anapongeza uamuzi wao wa kuamini Chadema ndio chama pekee kinachowafaa hivyo akaongeza wanakaribishwa na wapo tayari kushirikiana kukijenga na kuendeleza chama.