Vijana Lindi Watakiwa Kutobaguana

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akijumuika na wanachama wa Klabu Zalendo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kucheza wimbo wa ‘NANI KAMA MAMA’ muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi klabu hiyo inayoundwa na walimu, wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja wa wananchi mbalimbali katika Manispaa hiyo.  PICHA NA JOHN LUKUWI.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akijumuika na wanachama wa Klabu Zalendo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kucheza wimbo wa ‘NANI KAMA MAMA’ muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi klabu hiyo inayoundwa na walimu, wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja wa wananchi mbalimbali katika Manispaa hiyo. PICHA NA JOHN LUKUWI.

Vijana wa chipukizi kutoka Klabu Zalendo katika Manispaa ya Lindi wakionyesha michezo ya halaiki wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi wa klabu yao uliofanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye uwanja wa Ilulu tarehe 10.5.2015.

Vijana wa chipukizi kutoka Klabu Zalendo katika Manispaa ya Lindi wakionyesha michezo ya halaiki wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi wa klabu yao uliofanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye uwanja wa Ilulu tarehe 10.5.2015.


Na Anna Nkinda – Lindi

VIJANA mkoani Lindi wametakiwa kuwa wazalendo na kutobaguana bali wasambaze upendo na kujiona wote ni sawa kwa kufanya hivyo wataondoa chuki na kudumisha amani, mshikamano na umoja katika jamii inayowazunguka. Mwito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua klabu zalendo zilizopo katika Manispaa ya Lindi.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dk. Jakaya Kikwete alisema kama jamii itajenga tabia ya ubaguzi italeta chuki na upendo utatoweka na hivyo kusababisha vurugu zitakazopoteza amani iliyopo. Alisema uzalendo ni kiini cha maendeleo hivyo huwezi kuwa mzalendo kama hupingi rushwa na matumizi ya madawa ya kulevya, hutunzi mazingira, hushiriki kuchangia utoaji wa damu salama na kutokuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo katika jamii yako.

Mama Kikwete alisema, “Leo hii nimezindua klabu zalendo, Mzalendo ni mtu mwenye huruma na mtu anayeona thamani ya kitu alichonacho tunzeni vitu mlivyonavyo ikiwemo Amani ya nchi yetu na mjitoe kufanya kazi kwa bidii ili muweze kupata maendeleo.

Aidha Mama Kikwete aliwahimiza wanafunzi kujitendea haki kwa kusoma kwa bidii hadi elimu ya chuo kikuu kwa kufanya hivyo wataweza kuajiriwa na kujiajiri katika katika fani mbalimbali na kujiletea maendeleo katika mkoa wao wa Lindi.

Akisoma historia fupi ya klabu zalendo Mwalimu Mwajuma Malugu ambaye ni Mwenyekiti alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kuutetea na kuulinda muungano wa Tanganyika na Zanzibari ndiyo maana wanatumia namba za #26464# ikimaanisha tarehe 26 mwezi wa 4 mwaka 1964 siku ya muungano. Aliyataja malengo mengine kuwa ni kuhamasisha wanafunzi na vijana waliopo mtaani kuwa wazalendo na kuipenda nchi yao kwa kufanya hivyo wataepukana na mambo yasiyofaa kwa maslai ya nchi yao.

“Mafanikio tuliyoyapata ni kujenga umoja na ushirikiano, kuongeza idadi ya wanachama na hii inatokana na kufunguliwa kwa matawi mengine ya uzalendo mashuleni na mitaani, kuongeza na kupanua uelewa kwa wanafunzi na raia kuhusu klabu ya uzalendo, kuwahamasisha watu kuwa wazalendo na kujitoa katika uchangiaji wa damu, kupinga rushwa, madawa ya kulevya pamoja na kulinda Amani ya nchi.

Mwalimu Mwajuma alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uhaba wa fedha kwa ajili ya kuandaa makongamao na mabonanza yatakayosaidia kuimarisha harakati zote za klabu ya uzalendo na kushindwa kutuma wawakilishi katika mikutano na makongamano ya wanaklabu ngazi ya taifa. Pia kikundi kimekosa semina kwa wanaklabu hali inayoplekea wanachama kukosa uelewa wa kutosha kuhusu madhumuni ya klabu hiyo.

Klabu zalendo ilianzishwa na walimu wa Shule ya Sekondari Lindi katikati mwa mwaka jana hadi sasa inawanachama 1450 kutoka shule za Sekondari Mkonge, Angaza, Ngongo, Ng’apa, Chikonji, Mingoyo, Kineng’ene, chuo cha ufundi VETA na walimu wa shule za msingi pamoja na wanafunzi wao. Pia klabu hiyo imehusisha vijana kutoka mtaani wanaofanya kazi za udereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda, wavuvi na wanavikundi vya Sanaa.

Mama Kikwete aliahidi kukipatia kikundi hicho mipira 20 na jezi seti 10 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ambao watashiriki katika mashindano mbalimbali na kuangalia utaratibu wa kuwapatia mradi ambao utawasaidia kuwainua kichumi.