Kituo cha kukuza mchezo wa mpira wa Miguu kutoka nchini Kenya cha Trans Nzoia Youth Sports Association ( TYSA) kimetua Mkoania Arusha na kusaidia baadhi ya watoto ili kuwahamasisha katika mchezo wa Huo.
Ofisa wa kukuza michezo katika kituo hicho Francis Ojilo alisema kuwa wameamua kusaidia watoto ili kuhakikisha vijana wanakua na elimu ya michezo pamoja na nidhamu hivyo jamii nzima itanufaika na program ambayo wanaifanya.
“Tupo na watoto kutoka sehemu mbalimbali hapa Mkoani Arusha na tunawafundisha mambo tofauti tofauti kuhusu michezo na hata ya kijamii, Mfano tunamjenga mtoto kutambua kipaji chake na kuwasaidia katika nidhamu ya michezo” alisema Ojilo.
“Hatumfundishi mtoto jinsi ya kufunga tu, ila tunamfundisha jinsi ya kukaba, kutoa pasi na kuisaidia timu inapozidiwa na hata inapohitaji kulinda ushindi ambao wameshaupata”
Hata hivyo Ojilo alisema kuwa michezo husaidia kwa kiwango kikubwa kwa mtoto kuwa na akili nyingi hata kufanya vizuri akiwa darasani.
“Wazazi tunashirikiana nao vizuri kwa sababu huwa tunafanya mikutano mbalimbali na wazazi, na walimu kutoka shule ambazo watoto wanasoma hivyo kila mtu ananafasi ya kuhakikisha mwanae anafanikiwa” Alisema Ojilo.
TYSA wapo jijini hapa katika ushiriki wa tamasha la Zinduka lililoanza kufanyika alihamisi na kumalizika jumamosi, tamasha la Zinduka linashirikisha Nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
Ojilo aliongeza kuwa tatizo kubwa linalowakabili wanamichezo katika jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuwa na uongozi usiojua majukumu yao ipasavyo hasa ya kuendelea michezo na kutokuwa na ushirikiano mzuri na wadau mbali mbali wa michezo.