Vigogo wasababisha vurugu Loliondo

Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakimsukuma mgonjwa kwenye kiti cha magurudumu kuelekea kwa babu kupata dawa.

08 March 2011
Arusha

WATU wanaodaiwa kuwa ni vigogo wa Serikali wamesababisha vurugu kubwa katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo kunakotolewa tiba ya magonjwa ya sugu na Mchungaji Mstaafu, Ambilikile Mwasapile baada ya kuvuruga utaratibu wa foleni kabla ya kupata huduma hiyo. Vurugu hizo zilianza pale kundi la watu lilipobaini kuwa

vyombo vya dola, askari polisi na wanamgambo waliokuwa wanalinda usalama katika eneo hilo, wanawasaidia vigogo kuwahi kunywa dawa kwa kukwepa foleni.

Hali hiyo ilisababisha wananchi kupoteza imani na ulinzi huo na kuamua kuziba barabara zilizokuwa zinakwepa foleni kwa kutumia mawe na agogo. Hata hivyo, vigogo

hao waliamua kuacha magari yao na kuanza kuelekea nyumbani kwa Mchungaji huyo kwa miguu kitendo ambacho kiliwafanya wananchi kuamua kuvamia jiko linalotumika kutengeneza dawa hiyo na kuanza kuinywa bila mpangilio jambo lililosababisha utaratibu wa kutoa dawa kusitishwa kwa saa saba.

Vurugu hizo zilisababisha msongamano mkubwa na watu kutawanyika ovyo katika maeneo mbalimbali ya kijiji hicho kiasi cha kuharibu shughuli za kawaida za kila siku za wenyeji ambao nao walikerwa na hali hiyo kiasi cha kuamua kukata mabomba ya maji yanayotumika kutengeneza dawa kwa mchungaji.

Akizungumzia tukio hilo, Mchungaji Mwasapile alielezea kuchukizwa na vitendo vya watu kuvamia na kujinywea dawa bila utaratibu.

Tangu kutangazwa kwa habari za Mchunguji Mwasapile kutibu magonjwa sugu, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaomiminika kijijini hapo kutaka kupata huduma hiyo kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wamepoteza maisha hata kabla ya kuhudumiwa.
Uchunguzi uliofanywa umeonyesha kwamba wengi wa wagonjwa waliofariki dunia ambao wanakadiriwa kuwa kati ya sita na 14, ni wale waliotolewa wakiwa hoi katika hospitali mbalimbali nchini hasa za Kanda ya Kaskazini.

Akizungumzia tukio la wagonjwa kufariki wakiwa wanasubiri huduma, Mchungaji Mwasapile aliwataka wananchi kuacha kuwahamisha wagonjwa waliolazwa hospitalini na kuwapeleka kwake.

Alisema kitendo hicho kinasababisha wengine kuzidiwa na hata kufa kwa kuwa wanaotaka huduma ni wengi kuliko uwezo wa kuwahudumia mara moja. Alisema kitendo cha wagonjwa kukaa muda mrefu katika mazingira mabaya ya kusubiri dawa kunasababisha wengi kuzidiwa na hata kufa.

Akizungumza na Mwananchi jana, mmoja wa wasaidizi wa mchungaji huyo, Paulo Dudui alisema: “Mchungaji anawaomba watu wenye wagonjwa wachukuwe tahadhari ili wagonjwa wanaowaleta waweze kufika kwa mchungaji na kupata tiba. Wajue kuna wagonjwa wengi,

barabara ni mbaya  na huku hakuna huduma muhimu kama chakula. Leo nimeona miili mitatu ya wagonjwa waliofariki dunia.” Dudui alisema kutokana na taarifa ambazo wanazo kulikuwa na watu wengine sita ambao walifariki, akiwepo mtoto mdogo ambaye aligongwa na gari akiwa amelala.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali alisema taarifa alizonazo hadi juzi kulikuwa na vifo vya watu sita. Hata hivyo, baadhi taarifa zilizopatikana kutoka kwa waliokuwa wanasubiri kuhudumiwa zilisema waliokufa ni 14.
Hata hivyo, mmoja wa wafiwa aliyejitambulisha kwa jina moja la Rogers, mkazi wa Kigoma alisema baada ya kufiwa na ndugu yao yeye na ndugu zake walichukua uamuzi wa kumzika ndugu yao njiani: “Tulilazimika kushuka na kumzika njiani,” alisema Rogers wakati akiwa kwenye foleni ya kwenda kupata dawa akisema hata yeye ni mgonjwa.

Alisema baada ya kupata dawa itabidi arejee kwao kutoa taarifa za msiba huo ili taratibu nyingine za kifamilia zichukue mkondo wake. Baadhi ya wafanyabiashara wamevamia eneo hilo na kuanza kuuza bidhaa kwa bei ya juu. Bei ya maji ya nusu lita inayouzwa Sh500 inauzwa Sh1,000 na ya lita moja hadi moja na nusu yaliyokuwa yanauzwa Sh 1,000 yamefikia Sh. 2,500.

Sahani moja ya chakula iliyokuwa inauzwa Sh. 1,000 kijijini hapo, sasa inauzwa Sh. 2,500 hadi 4,000.  Kuku aliyekuwa anauzwa Sh. 6,000 sasa ni Sh. 25,000. Wilaya nayo imekuwa ikitoza Sh. 2,000 kwa kila gari linalopeleka wagonjwa huko, utaratibu uliobuniwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro kwa ajili ya kutengeneza vyoo na huduma nyingine muhimu ambazo zinahitajika.

Tayari, wafanyabiashara kutoka mkoani Kilimanjaro wameanza kupeleka mahema na huduma za vyakula katika kijiji hicho. Dudui, alisema kuwa tayari gari moja kubwa la mahema ya kukodi lilifika jana kijijini hapo na kazi ya kuyafunga inaweza kuanza leo.

Chanzo cha habari hii ni Gazeti la Mwananchi la Tanzania.