Vigogo wanaotaka urais waivuruga CCM Arusha

Na Janeth Mushi, Thehabari, Arusha

KAMATI  ya maadili na usalama  mkoa wa Arusha iliyoshirikisha wajumbe watatu kutoka makao makuu ya CCM na UVCCM  imeelezwa kuwa chanzo kikuu cha vurugu za vijana Arusha kuwa  ni mbio za kuwania urais mwaka 2015.

Inadaiwa kuwa  katika kamati hiyo wanachama wa UVCCM mkoa wa Arusha wamebainisha wazi kuwa jumuia hiyo hivi sasa inatumiwa na vigogo kwa ajili ya kujiimarisha katika mpango huo wa kuwania urais.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bermadi Membe,Mary Chatanda katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, na Godfrey Mwalusamba mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arusha ni majina ambayo yamehusishwa katika mpango huo

Wakizungumza  kwa masharti ya kutotajwa majina yao  baadhi ya viongozi wa jumuiya ya  vijana  wa chama hicho wamethibitisha kutajwa kwa majina hayo katika kikao hicho cha kamati ya maadili  na usalama.

Taarifa zaidi zinadai kuwa baadhi ya vijana waliohojiwa na kamati hiyo wametaja kuhusishwa katika vikao vilivyofanyika jijini Dar es salaam eneo la Mikocheni katika nyumba moja ya kifahari ambapo vijana hao waliieleza  kamati hiyo kuwa katika kikao hicho cha Dar es salaam waliandaliwa na tamko maalum la kutumia katika kuwashambulia baadhi ya makada wa CCM na kuelekezwa kuwa wakiwa mkoani hapa Chatanda ndiye atakayewasaidia kufanikisha mpango huo.

Imedaiwa kuwa wajumbe hao wawili wa UVCCM kutoka Wilaya ya Arumeru walibainisha wazi katika kamati hiyo mbele ya Chatanda kuwa hata walipotoka jijini Dar na kufika Arusha walilazimika kuripoti kwa katibu huyo wa chama mkoa kama walivyoelekezwa na kupokelewa na katibu huyo ambaye aliwapa maelekezo

Habari zinasema kuwa mara baada ya kutokea kutokuelewana katika baadhi ya mambo katika kukamilisha mpango huo vijana hao walijiengua katika mpango huo na kuwa sehemu ya vijana wengine ambao hivi sasa wanampinga katibu huyo na kutaka aondolewe Arusha kwa madai ya kukivuruga chama(CCM).

Mpaka jana saa tisa usiku kamati hiyo ilimaliza kuwahoji makatibu wa vijana kutoka Wilaya za Monduli, Karatu na Longido ambapo mara baada ya kutoka katika kikango hicho hawakuwa tayari kuzungumza lolote juu ya kilichojiri katika mahojiano hayo.

Aidha katika kikao hichoMwenyekiti wa vijana mkoa wa Arusha James Milya ambaye ndie alikuwa mtu wa kwanza kuhojiwa na kamati hiyo kwa zaidi ya saa tatu ambapo alitoka kimyakimya bila kuzungumza chochote na kuzima simu,ambaye ndiye alikuwa chachu katika kamati hiyo iliyoalazimu kubadili utaratibu wa mahojiano hayo ambapo ilitakiwa baada ya Millya wafuate makatibu wa Wilaya lakini ikalazimika kuhamia kwa wanachama wa jumuiya hiyo ambao ndio waliaminika vinara wa maandamano hayo.

Imeelezwa kuwa waliohojiwa na kuichanganya zaidi kamati hiyo ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa vijana Wilaya ya Arusha Ally Bananga, Ally Shabani maarufu Majeshi na mjumbe mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Nyiti kutoka Arumeru ambao hao ndio wanatajwa kutumiwa awali na kambi inayotajwa kuwa ni ya Waziri Membe katika mpango ulioratibiwa jijini Dar es salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kutoka katika mahojiano hayo Majeshi na Nyiti walisema kuwa wao wamelazimika kueleza ukweli juu ya mpango mzima katika kamati hiyo ili ijulikane nini kinachoendelea kwa hivi sasa ndani ya Jumuiya na Chama kwa ujumla.

Aidha kufuatia mkanganyiko huo unaoendelea ndani ya Jumuiya hiyo ya Vijana ni dhahiri  kuwa vita iliyopo ni ya safari ya urais wa 2015 katika ya makundi ya wana CCM ambao wanatajwa kuwania nafasi hiyo.