*WAFANYAKAZI WA HAZINA, TANESCO NA WIZARA YA NISHATI WAHUSIKA, NGELEJA ATHIBITISHA UCHUNGUZI KUFANYWA
SERIKALI inawachunguza baadhi ya maofisa wake waandamizi kwa tuhuma za wizi wa dola50 milioni za Marekani sawa na Sh86 bilioni, zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta mazito ya kuzalishia umeme kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), katika kipindi hiki nchi inapokabiliana na tatizo la uhaba wa nishati hiyo.
IPTL inayozalisha megawati 100 za umeme iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco), lakini utendaji wake umekuwa na mkanganyiko.Chanzo kutoka serikalini kililiambia gazeti dada la The East African la Februari 12, kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwamba baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Hazina na Tanesco, wanahusika katika mpango huo wa wizi.
Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alipoulizwa alijibu, “Ndiyo naweza kuthibitisha upo uchunguzi unaoendelea, lakini ndiyo kwanza upo katika hatua za awali.” Tayari taarifa za awali za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), zinaonyesha kumekuwa na maelezo yaliyokiuka utaratibu wa fedha zilizolipwa na Serikali kwa ajili ya usambazaji wa mafuta mazito kutoka kampuni za ndani.
Ukosefu wa nishati ya umeme unaoikabili nchi kwa sasa unaifanya Tanesco kulipa IPTL dola12 milioni za Marekani sawa na Sh19.2 bilioni kila mwezi, kwa uzalishaji wa megawati 60 badala ya megawati 100.
Mwaka 1995, Tanesco iliingia mkataba na IPTL, mkataba ambao uliihusisha kampuni ya nchini Malaysia , Mechmar Corporation na wawekezaji wa ndani, na VIP Engineering and Marketing Company kwa ajili ya kuzalisha megawati 100 kwa kutumia mitambo inayotumia dizeli kwa miaka 20.Katika mkataba huo, VIP ina hisa ya asilimia 30 na ile ya Mechmar ya Malaysia ikiwa na hisa ya asilimia 70.Serikali ilikubali kulipa kwa ajili ya uzalishaji huo kwa kuwa haikuwa na njia nyingine.
Mpango wa kuifilisi IPTLTayari hivi karibuni Mahakama iliamua IPTL ifiilisiwe na jukumu hilo lilikabidhiwa kwa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (Rita).Hata hivyo, baadhi ya benki zinazoidai IPTL ziliweka zuio mahakamani zikitaka kwanza kulipwa fedha zao ambazo kampuni hiyo ilikopa.
IPTL inakadiriwa kuwa na Sh200 bilioni zilizopo Benki Kuu (BoT) ambazo kama ikifilisiwa zingeangukia mikononi mwa Serikali. Kampuni hiyo imekuwa ikiitafuna Tanesco mabilioni ya shilingi tangu kuingia mkataba huo ambao umekuwa ukitajwa kama wa kifisadi, kuliko hata wa Richmond.
CHANZO: Mwananchi