Na Mwandishi Maalum, Mtwara
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameutaka uongozi wa Chuo cha Ufundi Stadi Kanda ya Kusini (VETA) kuwa tayari kupokea walimu na vifaa ya kisasa vinavyoletwa na wawekezaji kwa ajili ya sekta ya gesi na mafuta.
Rais ametoa kauli hiyo jana mkoani Mtwara alipotembelea chuo hicho kwa ajili ya kuwaeleza nafasi iliyopo na makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na wawekezaji waliopo Mtwara katika sekta ya gesi na mafuta nchini ambao wameshaanza shughuli za uchimbaji na utafutaji wa mafuta.
Katika makubaliano hayo wawekezaji hao watahitaji wataalamu mbalimbali katika shughuli zao na hivyo imeamuliwa kuwa wawekezaji walete wataalamu ambao ni walimu watakaowafundisha wakufunzi katika chuo cha VETA na pia walete vifaa vya kufundishia taaluma mbalimbali zitakazohitajika katika uwekezaji huo.
“Msiwawekee pazia, muwe tayari kuwapokea wakufunzi hao na vifaa kwa ajili ya kuwatayarisha vijana wetu kwa ajli ya ajira katika makampuni hayo”. Rais amesema.
Tayari wakufunzi kutoka Brazil na baadae Uingereza wataendesha mafunzo katika VETA, mkoani Mtwara wameshaanza mafunzo.
Kulingana na wawekezaji hao ambao baadhi yao ni British Gas ya Uingereza, Petro Bras ya Brazil na wengine wako mkoani Mtwara kwa ajili ya kuwekeza katika gesi na mafuta.
Leo asubuhi Rais pia ametembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Naliendele ambapo ameelezwa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo ambazo ni pamoja na utafiti wa korosho ambapo tayari aina ya mbegu 22 zimegunduliwa na kati ya hizo 16 zimesajiliwa. Shughuli zingine ni utafiti wa magonjwa, vipande (Agronomia) na uchumi jamii, utafiti wa magonjwa ambapo ni wadudu wa mihogo na utafiti katika kusindika.
Akizungumza katika kituo hicho, Rais amesema serikali imeamua kupunguza changamoto zinazokabili vituo vya utafiti hapa nchini “Nataka mwaka huu tufanye kazi ya kuviwezesha vituo vya utafiti, tutavikarabati na kuvipatia vifaa na pia kuongeza pesa kwa ajili ya utafiti na hatimaye utafiti huu uwafikie walengwa ambao ni wakulima” Rais amesema. Rais anaendelea na ziara ya Mtwara vijijini.