Vatican Yasifia Uhusiano wa Wazanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akifuatana na Balozi wa Vatican nchini Tanzania Francisco Mantecillo Padilla alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

Na Mwandishi Maalumu, Zanzibar

VATICAN imepongeza uhusiano na mashirikiano yaliopo baina ya wananchi wa Zanzibar ambao wamekuwa wakiishi pamoja bila ya kujali itikadi zao za kidini hatua ambayo imekuwa chachu ya kuimarisha amani, utulivu na maelewano. Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Francisco Mantecillo Padilla aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

Balozi Padilla ambaye amefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais, alieleza kuwa amani na utulivu pamoja na maendeleo yaliopatikana Zanzibar yamechangiwa zaidi na wananchi wake ambao wanakiishi kwa upendo bila ya kujali itikadi zao za kidini. Alieleza kuwa Vatican ina kila sababu ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kukuza uhusianoa na ushirikiano wake kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa maelewano makubwa ya watu wake.

Balozi Padilla, alisema kuwa Vatican itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo. Alisema kuwa Vatican itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya, elimu pamoja na huduma nyengine za kijamii.

Balozi huyo wa Vatican nchini Tanzania alimuahidi Dk. Shein kuwa Vatican itaendeleza uhusiano wake kwa kuitangaza Zanzibar katika medani ya utalii sambamba na kuzieleza sifa zake kwa waekezaji wa Vatican. Sambamba na hayo alieleza kuvutiwa kwake na mazingira ya Zanzibar ambayo ni kivutio kikubwa cha watalii.

Naye Dk. Shein alitoa shukurani kwa Balozi huyo mpya wa Vatican nchini Tanzania kwa ujio wake hapa Zanzibar na kueleza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake wa kihistoria na Vatican. Dk. Shein alimueleza Balozi huyo wa Vatican kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika mashirikiano baina ya wananchi wake ambao wamekuwa wakifuata dini tofauti lakini wameweza kuishi kama ndugu tena kwa muda mrefu bila ya kubughudhiana.

Akieleza historia kwa ufupi juu ya uwepo wa uhusiano na ushirikiano wa wananchi wa Zanzibar ambao wamekuwa wakifuata itikadi tofauti za kidini, Dk. Shein alisema kuwa hatua hizo zimeanza miaka mingi iliyopita ambapo hata watawala wa Zanzibar waliweza kuzikaribisha dini mbali mbali hapa nchini na kuweza kufanya kazi zao kwa amani.

Alisema kuwa Zanzibar imekuwa na watu wanaofuata dini mbali mbali ambao wanaendesha shughuli na ibada zao katika mazingira huru bila ya wafuasi wao kubughudhiwa hali ambayo ni ustaarabu na imeijengea sifa kubwa Zanzibar ndani na nje ya nchi. Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kulinda uhuru wa dini zote kama inavyoelezwa katika katiba zote mbili na kueleza kuwa Zanzibar inathamini uhusiano huo mwema uliopo.

Alieleza kuwa licha ya kuwa Tanzania haina dini ya serikali kama ilivyokuwa ikisisitizwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na viongozi wengine waliopita lakini bado Watanzania wengi wakiwemo Wazanzibari ni wafuasi na waumini wa dini zenye madhehebu tofauti..

Aidha, Dk. Shein, alieleza kuwa Serikali itaendeleza na kusimamia haki za Watanzania za kufuata na kuabudu dini waitakayo na kuishi bila ya kubaguana kutokana na sababu ya dini na huku akisisitiza kuwa Katiba zote ziko wazi juu ya hilo. Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar na Vatican pia, ipo haja kuzidsha uhusiano huo katika sekta ya elimu hasa elimu ya juu kutokana na Vatican kupiga hatua katika sekta hiyo na kuweza kupata mafanikio makubwa.

Sambamba na hayo, alieleza kuwa kutokana na Zanzibar kupiga hatua katika sekta ya utalii ambayo imekuwa ikiingizia fedha nyingi za kigeni na kuweza kuongeza pato la Taifa ipo haja kwa Vatican kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo. Pamoja na hayo, alieleza kuwa Zanzibar inawakaribishwa wawekezaji kutoka Vatican kuja kuekeza katika sekta mbali mbali ikiwemo hiyo ya Utalii. Balozi Francisco Padila anachukua nafasi ya Balozi Joseph Chenoth aliyemaliza muda wake wa kazi hapa nchini.