Uzingatiaji Masomo kwa Wanafunzi Suluhisho la Matumizi ya Madawa ya Kulevya

Haya ni baadhi ya madawa ya kulevya (Bangi)

Na Mwandishi Wetu, Hai

TATIZO kubwa la matumizi ya madawa ya kulevya hasa kwa vijana linaweza kumalizika endapo wanafunzi watajipanga vema katika masomo yao na kutumia elimu na maarifa wanayopata shuleni kwa ajili ya kujiendeleza kimaisha.

Changamoto hiyo imetolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Msufini, Bi. Eva Kira, kwenye sherehe ya mahafali ya 22 ya Kidato cha Nne katika shule hiyo iliyopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Bi. Kira alisema tatizo la ulevi na utumiaji wa madawa ya kulevya linaloikumba nchi kwa sasa, linatokana na wanafunzi wengi kutozingatia masomo hali ambayo inawasababishia kufanya vibaya katika matokeo ya mwisho na kuishia mitaani.

Alisema kitu kinachowafanya wanafunzi kufeli mitihani ni kupunguza hari ya kusoma hali ambayo imekuwa ikisababisha kupatikana kwa vijana wengi wa mitaani wasio na ajira ambao hujiingiza kwenye makundi maovu ikiwemo uvutaji wa Bhangi na utumiaji wa madawa ya kulevya ambayo huwapelekea kupata maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi.

“Tungependa kusikia na kuona wanafunzi wetu wanafanya vizuri na kuchaguliwa kuendelea na elimu ya juu, kwani hali hiyo itawapa nafasi kubwa ya kupata ajira na hata kujiajiri wenyewe, na hili pia litawasaidia kujinasua kwenye changamoto nyingi zilizopo kwa sasa kama vile ulevi, madawa ya kulevya, maambukizi ya ya ugonjwa wa ukimwi,wizi na ujambazi,” alisema Bi. Kira.

Akisoma risala ya kidato cha nne Hosea Mathias alisema pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika shule hiyo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vifaa vya maabara, vifaa vya michezo pamoja na ukosefu wa bwalo la chakula ambapo aliwaomba wadau mbalimbali wa elimu kujitokeza kuwasaidia ili kuweza kuondokana na matatizo hayo.

Akizungumza Mkuu wa pili wa jimbo la Hai la kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini chungaji Fuatael Munis, aliwataka wanafunzi kuepuka kuchanganya suala la mapenzi na masomo, kutokana na kwamba hali hiyo itawasababishia kuharibu malengo yao ya baadae ya kimaendeleo.

“Wanafunzi epukeni masuala ya mapenzi pindi muwapo shuleni, zingatieni kile mnachofunzishwa na walimu ikiwa ni pamoja na maadili, kwani mapenzi ni hatari sana shuleni hali hiyo itawafanya mfeli kimaisha ,someni kila jambo lina wakati wake,” alisema.

Jumla ya wanafunzi 74 katika shule hiyo ya Msufini inayomilikiwa na kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini,wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Oktoba 8 mwaka huu.