Na Anna Nkinda – Maelezo
MSICHANA mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni mjamzito au anamtoto idadi hii inawakilisha maisha yao halisi na kuonyesha kwamba kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa wasichana wataendelea kukosa haki zao za msingi na kuzidi kuwa wategemezi.
Hayo yamesema na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa utafiti katika ukunga ulioandiwa na LUGINA Afrika Midwives Research Network (LAMRN) uliofanyika katika Hoteli ya Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema vifo vya kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni tatizo katika nchi zote zilizopo Kusini mwa Bara la Afrika hata hivyo jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua au kumalizika kabisa.
“Naamini utafiti uliofanywa na LAMRN kwa kipindi cha miaka miwili utasaidia kuongeza utendaji kazi wa wakunga na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto katika bara letu la Afrika,” alisema Mama Kikwete.
Kuhusu mimba za utotoni Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema tafiti zilizofanyika zinaonyesha wasichana wanaanza kufanya mapenzi mapema zaidi wakiwa na umri mdogo ukilinganisha na wavulana jambo linalopelekea kupata mimba za utotoni na hivyo kukosa elimu kwa kukatisha masomo yao.
Mama Kikwete alisema, “Takwimu za Ulimwengu zinaonyesha zaidi ya wasichana milioni 58 wameolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 kati ya hao milioni 15 wanaumri wa miaka 10 hadi 14”.
Nchini Tanzania asilimia 13 ya wasichana wanaanza kufanya mapenzi wakiwa na umri wa miaka 15 na kwa upande wa wavulana kwa umri huo huo ni asilimia saba”. Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Paul Makonda alisema kauli mbiu ya mkutano huo ambayo ni utendaji wa kazi kwa kutumia ushahidi wa utafiti: utaimarisha afya ya mama na watoto wachanga imekuja wakati muafaka wa kuweka suala la afya ya mama na mtoto kwanza hii ni moja ya mipango ya shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa mwaka 2010-2015 katika bara la Afrika.
Makonda alisema hatua mbalimbali zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutoa wataalam kwa nchi wanachama ili waweze kupunguza vifo vya watoto na kuimarisha afya ya mama mjamzito.
“Ninategemea kwamba kwa kutumia ushahidi uliopatikana katika utafiti kwa pamoja tutaweza kutimiza malengo yetu kwa kuimarisha afya ya mama na watoto wachanga katika Bara la Afrika ninaamini mawazo na jitihada zenu zitaendelea ili kuleta mabadiliko katika sekta ya afya,” alisema Makonda.
Naye Dk. Rose Laisser ambaye ni msimamizi wa LAMRN nchini alisema wakunga wanahudumia asilimia 42 ya kina mama wajawazito wakati wa kujifungua hii ikiwa ni uwiano wa mkunga mmoja kwa wazazi 40 wakati katika hali halisi mkunga mmoja anatakiwa kuhudumia wanawake sita.
Dk. Rose alisema, “Pamoja na wakunga kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhudumia wajawazito wengi lakini bado wanafanya kazi kwa bidii na kujituma ya kuwahudumia kinamama na watoto wachanga”.
Chuo Kikuu cha Manchester cha nchini Uingereza na Partnerships for Global Health (THET) walitoa fedha kwa nchi sita Barani Afrika kwa kipindi cha miaka miwili ili wakunga 20 kutoka kila nchi waweze kufanya utafiti na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu kazi hiyo.
Jumla ya wakunga 120 kutoka nchi za Tanzania, Zambia, Malawi, Kenya, Uganda na Zimbabwe walifanya utafiti na kuwasilisha mambo waliyojifunza na changamoto walizokutana nazo katika mkutano huo. Mkutano huo wa siku nne ulihudhuriwa na wadau wa afya wakiwemo wakunga wapatao 220 kutoka Tanzania, Zambia, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Malawi, Uingereza, Sweden, Switzeland, India na Namibia.