Uwazi na Uwajibikaji Unawahusu Wote si Serikali tu-JK

Mkurudenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza Bw. Brian Eyakuze akimkabidhi Rais Jakaya Mrisho Kikwete tuzo maalumu ya taasisi zisizo za kiserikali kwake kwa kuwa kiongozi aliyetekeleza kwa vitendo masuala ya Serikali ya Uwazi na Ushirikiano. Hii ni wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Mei 20, 2015.

Mkurudenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza Bw. Brian Eyakuze akimkabidhi Rais Jakaya Mrisho Kikwete tuzo maalumu ya taasisi zisizo za kiserikali kwake kwa kuwa kiongozi aliyetekeleza kwa vitendo masuala ya Serikali ya Uwazi na Ushirikiano. Hii ni wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Mei 20, 2015.


Na Joachim Mushi

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema dhana ya uwazi na uwajibikaji haipaswi kutekelezwa na Serikali pekee, bali inawahusu pia waendeshaji wa asasi za kiraia ili kujenga imani kwa raia wote. Rais Kikwete amebainisha hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Open Government Partnership (OGP) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema dhana ya uwazi na uwajibikaji inawahusu wadau wote yaani Serikali na asasi za kiraia ambao ndio wadau wakuu wa OGP hivyo kuzitaka kutekeleza kila mmoja na si kuiangalia Serikali pekee.

“…Dhana ya uwazi na uwajibikaji inawahusu wadau wote yaani Serikali na asasi za kiraia ambao ndio wadau wakuu wa OGP. Tutakuwa tunakosea sana kama tutadhani kuwa dhana hizi mbili zinaihusu Serikali pekee. La hasha! Uwazi na uwajibikaji unazihusu pia asasi za kiraia. Lazima nao wawe wawazi kuhusu shughuli wazifanyazo ili jamii na watu wajue wanachokifanya kwa niaba yao, kwa ajili yao na jinsi wanavyowajibika kwao,” alisema Rais Kikwete.

Aidha alisisitiza kuwa suala la mapato na matumizi, lazima asasi za kiraia nazo ziwe wazi kuieleza jamii wamepata pesa kiasi gani, kutoka kwa nani, kwa ajili gani na jinsi walivyozitumia fedha hizo, ili jamii na wananchi ambao ndiyo walengwa wa shughuli za asasi hizo wanastahili kujua kwani fedha hizo zimetolewa kwa manufaa yao na siyo ya viongozi na watendaji wa asasi za kiraia.

Aliongeza kuwa tabia ya asasi za kiraia kukataa kuwa wa wazi na kuwa wakali wanapotakiwa kufanya hivyo siyo sahihi kwani ni kinyume na misingi ya Open Government Partnership, huku akisisitiza kuwa Kutokufanya hivyo ndiko kunakozua mashaka wakati mwingine hata mizozo.

“…Asasi za kiraia nazo lazima ziwe wazi na zitoe taarifa za shughuli ili wananchi ambao ndiyo walengwa waweze kujua kama kweli wamenufaika. Ili, pia, wananchi waweze kuhoji, kudai haki na kuwataka wahusika kuwajibika. Ni vyema ikaeleweka siku hizi sehemu kubwa ya fedha za misaada ya maendeleo hupitia asasi za kiraia hivyo kunapokosekana uwazi kupitia utoaji wa taarifa zilizo sahihi kuna hatari ya pesa za maendeleo ya wananchi kutokuwawafikia walengwa na kunufaisha watu wachache,” alisema Rais Kikwete.

Kauli mbiu ya Mkutano huu yaani “Kuimarisha Uwajibikaji Kupitia Uwazi katika Uendeshaji wa Shughuli za Serikali” (Enhancing Accountability Through Open Governance) ni maridhawa kabisa. Kuendeleza uwajibikaji Serikalini ndiyo shabaha kuu ya Mpango wa Uwazi katika Serikali.

Serikali kuendesha shughuli zake kwa uwazi ni jambo la msingi katika uwajibikaji. Wananchi ambao ndio walengwa na ndiyo sababu ya kuwepo kwa Serikali watatambua kwa uhakika jinsi serikali yao inavyowahudumia kama kuna uwazi. Uwazi unawawezesha watu kudai haki zao au kuwakumbusha viongozi na watendaji Serikalini kutimiza wajibu wao kwa raia wanaotakiwa kuwahudumia.