Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BARAZA Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), limelaani kitendo cha wajumbe wa Halmashauri Kuu NEC ya CCM kujilimbikizia madaraka. UVCCM imependekeza wajumbe wa NEC, wasiwe na madaraka zaidi ya moja kwenye maamuzi ngazi ya kitaifa.
Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa alitoa tamko hilo mjini hapa jana, katika mkutano na waandishi wa habari, alipokuwa akizungumzia maazimio waliofikia baada ya kumalizika kwa mkutano wa baraza hilo uliofanyika juzi na jana.
Malisema wajumbe wa NEC, hivi sasa wanatakiwa kuchaguliwa kutoka wilayani na kuongeza kuwa hiyo ni kwa wale ambao hawana madaraka mengine ya kitaifa.
“Lengo la kufanya hivi ni kutaka kurudisha chama kwa wanachama wenyewe na siyo mtu kuwa na vyeo kochokocho. Hivi sasa unakuta mtu mmoja ni Mbunge, Waziri, Diwani, Mwenyekiti wa Mkoa, MNEC, yupo kwenye Baraza la Wawakilishi, au ni Mwenyekiti wa Halmashauri.
Haya ndiyo tunataka kuyaondoa ndani ya chama chetu, haiwezekani mtu kuwa na nafasi za uongozi kiasi hicho, kitendo cha mjumbe kujilimbikizia madaraka kiasi hicho kinafanya hata uwajibikaji wake ndani ya chama uwe na wasiwas, hivyo haya tunataka yasiwepo kwenye uchaguzi ujao.
Malisema wamependekeza mtu anatakiwa kuchagua nafasi moja tu pindi itakapofika wakati huo na si kuwa ba mlindikano wa madaraka,” alisema Malisa.
Pia alisema baraza hilo limependekeza wajumbe wa NEC wa jumuiya wachaguliwe na jumuiya zenyewe na kwamba viongozi wa chama walio na nafasi za kushiriki katika maamuzi ya kitaifa wasipendekezwe kugombea nafasi za NEC.
Baada ya waandishi kumtaka aeleze kuhusu Mwenyekiti wa Chama ambaye ni Rais, alisema kwenye nafasi hiyo hawakuona tatizo lolote, hivyo nafasi hiyo itabaki kama ilivyo na kwamba haiathiri chochote.
Malisema akiendelea kuzungumza alisema, baraza hilo limekamilisha mchakato wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
“Mchakato wa kuwapa wagombea tumeukamilisha na tayari majina yamepatika ambapo tumetoa mapendekezo kwa kuwawekea alama wagombea wote na tumeyawasilisha katika ngazi ya juu kwa uamuzi wa mwisho. Tumependekeza uchaguzi huo ufanyike, mwishoni mwezi wa Oktoba mwaka huu.