*Asema ndicho kiini cha mpasuko, hali ndani ya chama si shwari
MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Benno Malisa, ameibuka na kudai kuwa wazee ndio kiini cha mipasuko na mivutano ya kisiasa ndani ya chama hicho na taifa, huku akionya kuwa hali ya kisiasa ndani ya chama hicho tawala kwa sasa si ya kuridhisha, kwani kimepoteza mwelekeo kutokana baadhi ya vigogo wake kushindwa kufanya maamuzi stahili katika kukijenga na kuondoa hali hiyo.
Malisa alitoa madai hayo mazito jana wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya, na kuwataka wazee ndani ya CCM kutumia busara, kujing’atua na kuwaachia vijana kukijenga chama hicho.
Akiwahutubia vijana wilayani Mbarali, Malisa alihoji sababu zilizowafanya wazee kuhofu mkusanyiko wa vijana wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni wakati wa vikao vya juu vya chama hicho.
Madai hayo ya Malisa yamekuja siku chache baada ya kumalizika vikao vya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC) ya CCM mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengi , awali ilidaiwa kwamba kulikuwa na mpango wa kuvunja uongozi wa UVCCM kutokana na malumbano yanayoendelea ndani ya Jumuiya hiyo muhimu kwa uhai wa chama hicho.
Kutokana na tetesi hizo, wakati vikao hivyo vikiendelea chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, viongozi wa UVCCM kutoka karibu mikoa yote nchini, walikusanyika mjini humo kufanya kile walichokiita “kupigania umoja wao na chama chao,” endapo hatua hiyo ingetekelezwa, hali iliyoonekana kuzidi kuchafua hali ya hewa ndani ya chama hicho kikongwe.
Taarifa zilieleza kwamba wenyeviti wa UVCCM kutoka mikoa 18 nchini, walikutana katika ukumbi wa baa moja maarufu iliyopo eneo la Area ‘D’ mjini Dodoma kupanga mikakati jinsi ya kuuokoa umoja wao usivunjwe na hatua za kuchukua iwapo azma hiyo ingetekelezwa.
Hata hivyo, vikao hivyo vilimalizika bila kuchukua hatua yoyote inayoonekana kuhatarisha uwepo wa UVCCM katika maazimio yake yaliyotangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama.
Makamu Mwenyekiti huyo wa UVCCM aliyekuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja akitokea mkoani Iringa, alisema hali ya kisiasa ndani ya CCM kwa sasa si ya kuridhisha, hivyo kupoteza mwelekeo kutokana baadhi ya vigogo wake kushindwa kufanya maamuzi stahili katika kukijenga na kuepuka mipasuko hiyo.
“Wazee sasa wamechoka kuongoza chama, ifikie wakati kufanya uamuzi wawaachie vijana, kukiongoza. Changamoto hii imekuja kwa wazee baada ya kuonyesha hofu kutokana na kikao cha vijana kilichofanyika mjini Dodoma na kujenga hoja isiyo ya msingi eti kuhoji, kulikoni vijana 6,000 kukutana? Walifadhiliwa na nani katika malazi na chakula? Wakati huo tukijaribu kuhoji fedha zinazotumiwa na chama ni nyingi kuliko hizo walizofadhiliwa vijana kushiriki kikao chao.” Alisema.
Rais Jakaya Kikwete
Alisema kuwa ni muhimu sasa vigogo ndani ya CCM kuachana na malumbano yasiyo na tija, badala yake kuweka mikakati ya kujenga Umoja na Vijana na siyo kujenga chuki baina ya UVCCM na Serikali inayoongozwa na CCM, hali aliyosema inapandikiza mizizi ya fitina isiyoleta tija ya maendeleo kwa taifa.
Alieleza kuwa wakati umefika sasa kwa vijana kupinga kwa kauli moja kutumiwa na wazee katika majukumu yoyote, badala yake wajenge umoja wa kuhakikisha wanaweza kufanya mabadiliko katika kuleta amani na kuijenga CCM kuwa imara.
“Daima nitasimama kwenye ukweli katika maslahi ya vijana na kwamba kuna baadhi ya wazee ndani ya chama ambao kwa makusudi wameamua kuendesha vita dhidi ya vijana na ‘kumwaga tindikali’ ili kuweza kuleta chuki baina ya viongozi na vijana wanaokipenda chama katika kuleta itikadi ya usawa na haki kwa Watanzania,” alisema.
Malisa alisema kuwa ni wakati wa vijana sasa kuanza mikakati ya kuwapumzisha wazee aliosema wameamua kwa nguvu moja ‘kuwamwagia vijana tindikali’ kwa lengo ya kuchochea umaskini kwa vijana wa Tanzania kwa kuwatumia vibaya kwa maslahi yao binafsi kisiasa.
Malisa alisema kuwa Rais Kikwete amekuwa na mitazamo mizuri dhidi ya wananchi wake na CCM, lakini kikwazo kikubwa ni watendaji wake kumzunguka na kumjengea mazingira yasiyoridhisha kwa wananchi.
Kiongozi huyo wa UVCCM alifafanua kuwa umoja huo tayari umetambua kuwepo kwa makundi ya watu wabaya, aliodai wanamzunguka kiongozi huyo wa nchi kwa kujengea fitina ili kujiandaa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Alibainisha kuwa ni wakati muafaka sasa wa kukaa na kutafakari njia bora ya kukiweka CCM katika hali ya usawa, kutafakari mbinu mbadala ya kutatua tatizo la ajira kwa vijana na kuondokana na mipasuko ya kisiasa inayochangia kudidimiza hali ya uchumi.
Alifafanua kuwa Serikali ilikiri kuwa kuna tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kwamba ni muhimu changamoto hiyo ikaangaliwa kwa makini ili kuhakikisha vijana wanapata ajira na kuweza kuwapumzisha wazee kukiongoza chama katika itikadi za kisiasa na kuondoa ubaguzi na mipasuko iliyopo ndani ya CCM.
“Ni vema viongozi wetu wa Serikali wakaelewa kwamba hatuwezi kutambua kama nchi iko imara na salama wakati vijana wenzetu wakiwa katika hali duni. Katika hali hiyo UVCCM ipo tayari kulaumiwa,” Malisa alisema.
CHANZO: Mwananchi