UVCCM Arumeru Wamdindia Mwenyekiti UVCCM Mkoa Arusha

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arumeru, Boniface Mungaya akizungumza na waandishi mara baada ya baraza hilo kukutana jana.

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arumeru, Boniface Mungaya akizungumza na waandishi mara baada ya baraza hilo kukutana jana.

 

 

Na Woinde Shizza, Arusha

BARAZA la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Arumeru limelaani kitendo cha Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai Sabaya kumsimamisha Kamanda wa Umoja wa Vijana wa UVCCM wilaya ya Arumeru, Mathias Manga kwa kile kuisaliti CCM katika uchaguzi mkuu wa mwa Oktaba 25 mwaka jana.

Baraza hilo limelaani tamko lililotolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai Sabaya na kumtaka ajitathmini na kujipima kama anafaa kuendelea kuwa mwenyekiti wa mkoa, kama ataona hawezi ajiengue mwenyewe.

Akizungumza na waandishi mara baada ya baraza hilo kukutana, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arumeru, Boniface Mungaya, alisema kuwa bado wanamtambua Manga ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya taifa (NEC), kama Kamanda wao wa vijana.

“Tunalaani tamko lililotolewa na Mkoa na hatumtambui kamanda mwingine, Kamanda wetu hajatendewa haki, wajumbe wa baraza la tumetathmini tamko la Lengai tunaona ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni,amepoka madaraka yasiyo yake, kitendo ambacho ni kurudisha chama nyuma badala ya kukijenga,” alisema na kuongeza; “Sabaya ajitathmini, ajipime kama anafaa kuendelea kuwa mwenyekiti wa mkoa kwani tunaona akiendelea kukiuka kanuni, atakiua chama, ni bora ajing’oe mwenyewe kama hawezi, tunampa siku saba akanushe madai aliyoyatoa dhidi ya kamanda wetu.”

Aidha alisema kuwa tamko hilo ni batili na hawalitambui na kumtaka Manga asivunjike moyo aendelee na haratkati za kukijenga chama hivyo asirudishwe nyuma na changamoto anazokabiliana nazo.

Akizungumzia yeye kuwepo kwenye baraza hilo alidai kuwa siku ya kikao alikuwepo ila alikataa kupiga kura ya kumkataa Kamanda wake na kuamua kutoka nje.

Naye Anjelina Lukumay ambaye ni mjumbe wa baraza hilo kutoka Kata ya Oldonyosambu, alimuomba Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa, Lekule Laizer kuliangalia suala hilo na kulitafutia ufumbuzi kwani Sabaya amekiuka kanuni za chama.

“Mwenyekiti wa wilaya ametumia kanuni ipi kumkataa kamanda wetu bila kutushirikisha? hatutakubali kuvurugwa wilaya ya Arumeru, tumepokea kwa mfadhaiko kauli hiyo kwani Sabaya kachaguliwa hata miezi miwili hana ila inakuwaje anataka kumtoa Manga tena bila kutushirikisha? alihoji Anjelina.

Wiki iliyopita uamuzi wa kumsimamisha Manga ulifikiwa katika kikao cha baraza la UVCCM Mkoa wa Arusha kilichozinduliwa na kaimu katibu mkuu Shaka Hamdu Shaka, ambapo kikao hicho kilikuwa na wajumbe 34 huku 33 kati yao wakipiga kura za ndiyo.

Pia kikao hicho kilitoa onyo kali kwa kamanda wa UVCCM wilaya ya Arusha Mjini, Longido na Monduli na kuwataka wajipime na kujitathimini kama wanatosha kuwa makamanda wa UVCCM na wakiona hawatoshi tunaomba wakae pembeni kabla baraza halijawachukulia hatua.

Uamuzi wa kumsimamisha Manga ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya taifa (NEC) wilaya ya Arumeru ulifikiwa.

Akisoma tamko lilitolewa na Kikao hicho cha baraza Katibu wa Hamasa wa (UVCCM) Mkoa wa Arusha, Lucas Nsomi alisema, Manga kuanzia wakati huo si kamanda wa Vijana Wilaya ya Arumeru tena kwani amepoteza sifa baada ya kudhibitika kukisaliti chama kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwani wakati wa uchaguzi huo alionekana akifanya vikao
vya kufanikisha ushindi kwa UKAWA.

“Kikubwa alichofanikiwa Manga ni kuwagawa vijana wa Arumeru hali inayopelekea kushindwa kuijenga jumuiya hiyo na kuanzia sasa sio kamanda wa vijana tena wa wialaya hiyo na sipo tayari kufanya naye kazi yoyote ile ndani ya CCM”.
Sabaya alidai kuwa vijana waliompitisha kuwa kamanda lilikuwa ni genge la wahuni ambao walikuwa wakiendesha vikao vya vijana wenye njaa na kwamba hayupo tayari kuwa Mwenyekiti wa magenge ya vijana wenye njaa na wasaliti ndani ya CCM.