Na Rajab Mkasaba, Ikulu-Zanzibar
UTURUKI imeahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Zanzibar hasa katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo elimu, kilimo, afya na utalii na kueleza kuwa itahakikisha mafanikio yaliokusudiwa yanapatikana.
Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davutoglu, aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo pamoja na kujitambulisha kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Davutoglu alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itahakikisha makubalizo yaliofikiwa katika kuimarisha sekta hizo za maendeleo kati ya viongozi wa nchi hiyo akiwemo Rais Abdullah Gul wakati Dk. Shein alipofanya ziara yake nchini huko mwaka jana yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Alisema kuwa Uturuki itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kutambua juhudi zake kuwa inazozichukua katika kuimarisha sekta zake za maendeleo.
Alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya elimu kumekuwa na mashirikiano mazuri kati ya nchi hiyo na Zanzibar hasa kupitia Chuo chake Kikuu cha Taifa cha SUZA ambapo tayari mchakato wa mashirikiano unaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu mbali mbali za kitaaluma.
Alieleza kuwa miongoni mwa program hizo ni pamoja na kubadilisha taaluma na wataalamu sanjari na kukiimarisha chuo hicho kwa kuongeza nyenzo za mafunzo.
Balozi Davutogla alimueleza Dk. Shein kuwa kwa upande wa sekta ya kilimo nchi yake itaendeleza mashirikiano katika kuhakikisha kuwa utaalamu wa uimarishaji wa kilimo uliofikiwa nchini humo pia, unawafikia na wataalamu wa hapa Zanzibar kwa kutoa mafunzo na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kukuza sekta hiyo hapa nchini.
Aidha, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa kwa upande wa sekta ya afya kumekuwa na mashirikiano mazuri ambapo tayari mchakato wa mashirikiano umeanza vyema ambao utasaidia kupata mafunzo na uzoefu madaktari wa Zanzibar pamoja na vifaa. Pia, balozi huyo aliahidi kuunga mkono juhudi za serikali za kuanzisha kitengo cha kushughulikia maradhi yatokanayo na matatizo ya figo, moyo, saratani na huduma nyenginezo.
Akizungumzia kuhusua sekta ya utalii, Balozi huyo alieleza kuwa kutokana na nchi yake kupata mafanikio katika sekta hiyo huku akiiona Zanzibar pia, ikipata mafanikio kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kutasaidia kuimarisha sekta hiyo hasa katika ukanda wake wenye vivutio vya kitalii huko Antalya ambako wataalii milioni 10 hufika kwa mwaka.
Naye Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi na shukurani kwa Balozi huyo pamoja na nchi yake ya Uturuki kutokana na azma ya nchi hiyo kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo hasa elimu, afya, kilimo, utalii na nyenginezo. Katika mazungumzo yake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na nchi hiyo na kusisitiza kuwa utaimarishwa na kuendelezwa kwa manufaa ya pande zote. Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini makubwa ya kufikia malengo yaliokusudiwa katika kuendeleza uhusiano huo hasa katika sekta hizo za maendeleo ambapo mchakato wake umeanza vizuri.
Akieleza juu ya mafanikio yaliopatikana katika sekata ya utalii, Dk. Shein alisema kuwa nchi hiyo tayari imefanikiwa katika sekta hiyo hasa katika Jimbo lake la Antalya ambalo limekuwa likitembelewa na watalii wengi kwa mwaka hivyo kuwepo kwa safari za ndege za Shirika la Turkish kati ya Antalya na Zanzibar kutapelekea watalii wengi kuja nchini.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na nchi hiyo kupitia Ubalozi wake wa Tanzania hapa nchini kuwa zitasaidia katika sekta hiyo za maendeleo na hata kuimarisha uekezaji na uhusiano wa Wafanyabiashara, wenyeviwanda wa Zanzibar na nchi hiyo.
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Burundi nchini Tanzania Bwana Issa Ntambuka aliyekujankujitambulisha ambapo katika mazungumzo yao walieleza haja ya kukuza uhusiano na ushirikiano katika sekta za maendeleo hasa elimu.
Balozi huyo wa Burundi nchini Tanzania, alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake ina mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar kwani kumekuwa na historia ya muda mrefu kati ya Burundi na Zanzibar. Naye Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar itahakikisha inampa ushirikiano wa kutosha ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi hapa Tanzania. Dk. Shein pia, alifanya mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Italia, James Alex aliyefika Ikulu kwa ajili ya kumuaga.