Utumishi Zanzibar wamuunga mkono Dk Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Na Rajab Mkasaba, Zanzibar

WIZARA ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeahidi kuunga mkono juhudi na bidii anazochukua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika kufanikisha maendeleo ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira bora Watumishi wa Umma na kuimarisha Utawala Bora.

Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, uliyasema hayo katika kikao maalum na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika muendelezo wa kukutana na Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia mpango kazi wa Wizara na uhusiano wa MKUZA na Dira ya 2020.

Katika Kikao hicho Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dr. Abdulhamid Yahya Mzee walishiriki.

Ukieleza mikakati iliyojiwekea, Wizara hiyo ikiwemo ile ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2011/2012, ukiongozwa na Waziri wake, Haji Omar Kheir, ulieleza kuwa miongoni mwa malengo yake ni kuimarisha ubora wa nguvu kazi na kuweka mazingira mazuri ya kazi.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa una malengo ya kuandaa mazingira bora kwa ukuaji wa uchumi na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maendeleo na tathmini ya sera za Serikali.

Pamoja na malengo mengineyo Wizara hiyo ilieleza kuwa ina malengo ya kuimarisha Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa kwa kuratibu utekelezaji wa programu ya mageuzi ya Utumishi wa Umma sanjari na kuimarisha utoaji wa huduma bora na kuendeleza amani na utulivu.

Wizara pia, imo katika hatua za mwisho kuanzisha Kamati ya Kitaifa ya Utawala Bora ambayo itasimamia na kuimarisha utekelezaji wa misingi ya Utawala Bora katika sekta mbali mbali za umma kwa ajili ya kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji.

Kwa upande wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Wizara ina lengo la kuongeza uwezo wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu katika ukaguzi pamoja na kusimamia matumizi mazuri ya fedha kwa uwazi na uwajibikaji.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Wizara ulieleza hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa jengo la Chuo cha Utawala wa Umma liliopo Tunguu na kueleza haja ya kuzidishiwa eneo la ardhi kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho kwa hapo baadae.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi zake kwa uongozi wa Wizara hiyo akiwemo Waziri wa Wizara hiyo kwa kusimamia vizuri Wizara hiyo pamoja na watendaji wake akiwemo Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na watendaji wengine kwa juhudi zao licha ya upya wa Wizara hiyo.

Aidha, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa kazi kubwa iliyopo mbelel yao ni kusimamia na kutekeleza malengo yaliopangwa ili irahisishe suala zima la kuandaa ripoti kwa yale yaliofanyika kwa robo mwaka hapo baadae.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alisisitiza umuhimu wa kuwa na eneo kubwa zaidi la Chuo hicho huko Tunguu kwa lengo la mahitaji ya hapo baadae kwani chuo kina matarajio ya kujiimarisha zaidi.

Mapema Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Kiongozi Dk. Abdulhamid Mzee aliueleza uongozi huo kuwa kuna umuhimu wa watendaji wa Wizara hiyo na uongozi wake wawe mfano katika kuwaongoza watumishi wengine wa serikali ikiwa ni pamoja na kulipa kipaumbele suala la kufika mapema kazini pamoja na kufuata taratibu na sheria za kazi.