MWENYEKITI wa Umoja wa Watanzania nchini Ujerumani Bw. Mfundo Peter Mfundo anayofuraha kubwa kuwakaribisha watanzania na marafiki wa Tanzania kutoka pembe mbali mbali za Dunia katika maadhimisho Sherehe ya Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani, zitakazofanyika mjini Koloni Ujerumani, Jumamosi ya Aprili 27, 2013 kuanzia saa 08:00 za mchana hadi usiku wa manane.
Katika sherehe hio ambayo imedhaminiwa na Umoja wa Watanzania Ujerumani (UTU) kushirikiana na culture center ya sarakasi. Die Zirkus Fabrik, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa za Tanzania, na atakayependa anaweza pia kununua bidhaa hizo. Ngoma za asili kutoka Tanzania, Mwanamuziki Kongwe Bi. Tabia Mwanjelwa naye atakuwepo, Msanii wa Bongo Flava Shah Smooth mwenye maskani yake Dublin.
Kikundi cha Sarakasi kitafanya mavitu yake ‘Live’ na mwisho Watanzania na wageni wote watapata fursa ya kuduarika na midundo kutoka Tanzania kupitia DJ Sudi Mnete wa DW. Akihojiwa na vyanzo vyetu vya habari Mwenyekiti, Bw. Mfundo Alisema, madhumuni ya sherehe hiyo sio tu kusherehekea Siku Kuu ya Muungano pekee, bali kutimiza moja ya maazimio ya UTU yaani kuwakutanisha Watanzania wanaoishi nchini humo.
Alisema lengo lingine ni kutangaza utamaduni wa Tanzania kwa watu wa Ulaya. “Moja ya agenda ya UTU ni kuhakikisha Watanzania wanaoishi nchini Ujerumani wanakuwa pamoja kwa hali zote, wanashirikiana kwa karibu na kusaidiana,” alisema.
Aidha aliongeza kuwa lengo lingine ni kuhakikisha wasanii wanaoisha Ujerumani wanatangaza kazi zao hadharani na wanazitumia kazi hizo kujipatia manufaa zaidi, alisema katika sherehe hiyo UTU imealika wasanii mbalimbali kuja kuonesha kazi zao.
Mwenyekiti aliwashukuru wasanii na Watanzania ambao tayari wameshajiandikisha kushiriki katika sherehe hiyo kubwa Mjini Koloni. “…Umoja ni Nguvu! KARIBUNI SANA MJINI KOLONI,” alisema