UTPC Yakabidhi Vifaa vya Kazi kwa Waandishi wa Habari

Katibu Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Beldina Nyakeke akipokea vifaa hivyo.

Na Pascal Buyaga wa Binda News, Musoma

JUMLA ya sh. milioni 800 zimetumika kununua vifaa vya vilabu 23 vya waandishi wa habari Tanzania Bara na Zanzibar vilivyoanza kutolewa na Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa lengo la kuwaongezea ufanisi wa kazi zao. Tayari vifaa hivyo vimetolewa kwa mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera imekuwa ya kwanza kukabidhiwa seti 13 ya vifaa hivyo kila mmoja.

Hafla hiyo ya makabidhiano ya vifaa katika ofisi za UTPC jijini Mwanza ambapo Rais wa UTPC, Keneth Simbaya alikabidhi vifaa vyenye thamani ya milioni 105 kwa vilabu vitatu vya Mwanza, Mara na Kagera ambapo kila klabu thamani yake ni milioni 35.

Kiongozi huyo amewataka waliovipokea vifaa hivyo kuhakikisha vinatumiwa kwa makini na wanachama wote na si kuhoziwa na viongozi tu wa vilabu, hata hivyo ameshauri iwekwe mipango mikakati itakayowawezesha kujitegemea vilabu ikiwa ni pamoja na kubuni miradi endelevu.

Awali Rais alisema UTPC ilianzishwa kwa madhumuni ya kuimarisha vilabu vya waandishi wa habari nchini, kuchangia kuleta maendeleo ya taifa sambamba na kuimarisha demokrasia nchini. “Ili mwandishi wa habari aweze kufanya kazi suala la uhuru ni muhimu sana, ukibanwa utakuwa katika kipindi kigumu ndicho tunachokipigania utpc alisema simbaya.”

Alisema kuwa vifaa hivyo vinalenga kuwa endelevu katika kazi ambapo wanahabari watafanya kazi kwa uhuru na kuhimili matakwa yao ya kila siku tofouti na awali kuwazimu kuazima kwa baadhi ya wadau.

“Sisi waandishi wa habari tunadhamana kubwa katika jamii lakini matendo yetu hayaonyeshi taswira nzuri katika jamii, tuwe mfano katika jamii ili tuweze kuwa kama mhimili wa nne wa Serikali,” alisema.

Aidha alionya tabia ya baadhi ya waandishi wa habari walioanza kugawanyika kwa kuegemea upande mmoja badala ya kuwa pande zote kwani kazi ya mwandishi wa habari kuielimisha jamii ili kuleta mabadiliko ya nchi kwa kuikomboa jamii inayoteseka vijijini na si kugawanyika kunakopelekea nchi kufika pabaya .

Vifaa vilivyokabidhiwa ni seti 13 kwa kila vilabu vilivyohudhuria hafla hiyo kila klabu imepatiwa Desktop Computer, Printer, Laptop, UPS, Binding Machine, Lamination Machine, Photocopy machine, Multimedia Projector, Collapsible Screen, Professional Still Picture Camera, Digital Tape Recorder, DVD Player na Seti ya TV.