UTPC Waunda Mfuko wa Mwangosi (Mwangosi Foundation)

Wanaharakati waandamana kupinga mauaji ya Mwangosi na kufungiwa kwa Mwanahalisi


Baadhi ya wanaharakati wakiwa wamebeba mabango ya jumbe mbalimbali kupinga mauaji ya Mwangosi


Baadhi ya wanaharakati wakiwa katika Kongamano la kupinga mauaji ya Mwangosi kwenye viwanja vya TGNP


Markos Albania (aliyesimama mwenye kipaza sauti) akizungumza na wanakongamano hilo.

UMOJA wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) unakamilisha taratibu za kuanzisha Mfuko wa Mwangosi (Mwangosi Foundation) ambao licha ya kuwa na majukumu ya kuisaidia familia ya Daud Mwangosi aliyeuwawa akitekeleza majukumu yake hivi karibuni mkoani Iringa, utakuwa na kazi ya kuwasaidia wanahabari wengine ambao watapatwa na matatizo kama yaliompata Mwangosi.

Taarifa ya kuanzishwa kwa mfuko huo huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) na Makamu wa Rais wa UTPC, Jane Mihanji alipokuwa akielezea mazingira ya kuuwawa kwa Mwangosi katika Kongamano la Wanaharakati waliokutana kupinga vitendo vya mauaji anuai yanayofanywa na Jeshi la Polisi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano (SJMC), Ayoub Rioba (kulia) akiwa meza kuu ya Mkutano wa Kongamano hilo pamoja na viongozi wengine.


Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (wa kwanza kushoto) akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevilli Meena. Kulia ni Mkurugenzi wa Gazeti la Mwana Halisi, Sued Kubenea (mwenye miwani).


Mihanji alisema tukio la mauaji ya Mwangosi ambalo limefanywa kinyama litaendelea kulaaniwa na kuwa chachu ya mabadiliko na utendaji wa nguvu wa wanahabari katika kazi zao. “Mwangosi Foundation mbali na kusaidia familia ya mwanahabari huyo utakuwa na kazi ya kuwasaidia waandishi wengine wanapokuwa katika matatizo yanayofanana na hayo,” alisema Mihanji ambaye pia ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi kutoka Gazeti la Uhuru.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Tanzania Tunayoitaka, Markos Albania alisema hali ya nchi kwa sasa ni tete kutokana na taarifa za mauaji ya mara kwa mara yanayotokea bila hatua stahiki ya kuthibiti kufanywa.

Alisema ni hatari hali kama hiyo kuachwa iendelee kwani sasa imefikia hatua hata wanahabari wanauwawa wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao, hivyo kuitaka Serikali kuhakikisha inasimamia sheria ili wanaohusika na mauaji ya Mwangosi wachukuliwe hatua inayostahiki.

“Ukimuua mwandishi umeuwa vyombo vya habari…ukiona Serikali inauwa wanahabari ujue ni Serikali mfu,” alisema mwanaharakati huyo. Aidha aliwataka Watanzania wote kuhakikisha wanasimamia na kupata Katiba Mpya na sio iliyopo sasa kwani imeshindwa kuwawajibisha baadhi ya viongozi wa Serikali wanaokwenda kinyume,” alisema Albania.