Na Mwandishi wa Thehabari Korogwe Vijijini
UTORO wa kudumu kwa idadi kubwa ya wanafunzi wa Sekondari hasa zile za Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe unatishia maendeleo ya elimu eneo hilo. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi juzi kwa baadhi ya sekondari umebaini hali hiyo sasa inatisha kwani inaongezeka kwa kasi karibuni katika kila shule za sekondari eneo hilo.
Katika sekondari za Kwagunda, Kwashemshi, Mulungui pamoja na Bungu vitendo vya utoro wa kudumu kwa wanafunzi vinaongezeka kwa hali ya juu jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya elimu eneo hilo. Akizungumzia hali ya utoro, Mwalimu wa Taaluma wa Sekondari ya Kwagunda, Halila Mohamed alisema shule hiyo hupokea wanafunzi 180 wanaojiunga kidato cha kwanza kila mwaka lakini wanaofika kidato cha nne ni 80 pekee, huku idadi kubwa wakiishia kutoroka.
Alisema idadi kubwa ya watoro hukimbilia kufanya vibarua katika machimbo ya matofari ya kuchoma kijijini hapo huku wengine wakifanya vibarua kwa wakulima na wafugaji wanaozunguka eneo hilo.
“Kibaya zaidi hutoroka na baadhi yao kuonekana kwenye mitihani tu…kimsingi mwamko wa elimu eneo hili bado upo chini sana kwa wanafunzi wenyewe pamoja na wazazi wao…,” alisema Bi. Mohamed.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwashemshi, Ezra Gweya alisema kipindi cha kilimo idadi kubwa ya wanafunzi shuleni kwake hukimbilia mashambani jambo ambalo huathiri maendeleo ya taaluma shuleni hapo.
“Utoro hapa shuleni kwetu upo, wengine huamua kutoa taarifa kabisa shuleni kwamba wanaandaa mashamba ya wazazi wao kwa ajili ya kilimo…wakati mwingine ukiangalia wanasema wanategemea kilimo kwa kipato hivyo wanalazimika kwenda mashambani,” alisema Gweya.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli alisema kati ya Januari hadi Juni 2012 shule yake ina jumla ya wanafunzi 226 kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne ambao ni watoro wa kudumu.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlungui iliyopo Kata ya Bungu wilayani Korogwe, Sylvester Msigwa alisema idadi kubwa ya wanafunzi watoro wanaishi peke yao kwenye ‘mageto’ hivyo kuwa na uhuru mkubwa.
“Wanafunzi hawa huwa na uhuru kupindukia, pia wanakuwa hawana nidhamu kwasababu wanakuwa mbali na walimu..hii ni changamoto kubwa sana..lakini natoa wito kwa wale wanaowapangisha wanafunzi nao wabebe jukumu la kuwalea wale watoto ipasavyo, wakiona mtoto anakwenda kinyume na maadili wawakemee,” alisema Msigwa.