Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
MANISPAA ya Ilala imevuka lengo la kutoa chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubella kwa watu 468,297 ambapo awali lengo lao lilikuwa kutoa chanjo hiyo kwa watu 445,801 wakati wa wiki ya kutoa chanjo hiyo nchini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Ilala Dk. Willy Sangu leo jijini Dar es salaam alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi la chanjo hiyo linalofanyika nchi nzima. Dk. Sangu alisema kuwa zoezi la kutoa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella linaendelea vizuri katika Manispaa ya Ilala kama ilivyopangwa ambapo linafanyika kwa muda wa wiki moja katika kote nchini.
“Ninawaomba watu wote ambao hawajajitokeza kupata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella, wafike kwenye vituo vya kutolea chanjo hiyo ili kuokoa maisha ya watoto, akina mama wajawazito, akiba baba na vijana,” alisema Dk. Sangu.
Dk. Sangu alisema kuwa idadi ya watu walioitikia wito wa kupata chanjo hiyo imekuwa kubwa katika Manispaa ya Ilala suala ambalo linawapa faraja ambapo watu wa rika zote wamejitokeza kupata huduma. Ili kutoa huduma ya chanjo kwa wakati kulingana na ratiba, Dk. Sangu amesema kuwa imewalazimu kuongeza vituo 30 ambapo timu ya wahudumu kutoka kwenye vituo mama inatoka ili kuwafuata wananchi waliko.
Awali Manispaa ya Ilala ilitenga vituo 236 vya kutoa chanjo hiyo kwa wananchi ndani ya Manispaa hiyo. Dk. Sangu amesema kuwa mafanikio idadi kubwa hiyo ya mwitikio wa watu kupata chanjo katika manispaa ya Ilala yanatokana na sifa ya kuwa katikati ya jiji ambapo watu wengi hupata huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake Afisa Muuguzi Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Ilala Queen Lutufyo amesema kuwa mwitikio wa watu kuja kupata chanjo ni mzuri na hawajakosa wateja muda wote wakati wa kutoa huduma hiyo kituoni hapo.
Aidha, katika zoezi la kutoa chanjo hiyo magonjwa ya Surua na Rubella wahudumu pia wanatoa dawa za magonjwa ya matende, mabusha, minyoo na matone ya vitamin ‘A’. Muda wa kutoa huduma hiyo ya chanjo vituoni ni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni licha ya kwanba wakati mwingine huduma hiyo hutolewa hadi saa 1:00 usiku kulingana na idadi ya wateja waliopo katika kituo wakati huo kuanzia Oktoba 18 hadi 24 mwaka huu.
Zoezi la kutoa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella nchini linaongozwa na kauli mbiu inayosema “Linda, Okoa, Zuia ulemavu- Kamilisha Chanjo” na kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Kusaidia Watoto (unicef), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Misaada la Marekani (UNSAID) na Muungano wa watoa chanjo duniani (Gavi).