Utapeli waendelea kwa ‘Babu’ Loliondo

 

Babu Mwasapila wa Loliondo

 

Na Janeth Mushi,  Thehabari 

Arusha

 SERIKALI mkoani hapa imetoa onyo kali kwa baadhi ya watu  wanaoghushi mihuri ya vibali vya magari yanayopeleka wagonjwa kijijini Samunge kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila  na kuviuza kinyume cha kanuni na sheria.

Onyo hilo limetolewa leo na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kufuatia baadhi ya watu kujitokeza ambao wamekuwa wakighushi mihuri ya Serikali na kuuza vibali kwa wasafirishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Yotham Ndembeka, alisema kuwa wamebaini kuwepo kwa vibali hivyo batili baada ya mkazi mmoja kutoka mjini Mbeya kudai ameuziwa kibali sh. 50,000.

“Tumebaini ubadhirifu huo baada ya mkazi mmoja toka mkoani Mbeya, kuleta malalamiko katika ofisi yetu baada ya kuuziwa kibali feki kwa sh. 50,000 katika eneo la chini ya mti na vibali vya kwenda kwa Samunge vinatolewa bure katika kituo kilichopo eneo la Kilombero mjini hapa na haviuzwi,” alisema.

Ofisa huyo alitoa wito kwa wasafirishaji na abiria kuwafichua wale wote wanaoghushi vibali ili kuweza kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Ndembeka alibainisha kuwa kuanzia sasa kuna madaftari maaluma ya Serikali ambayo yatakuwa katika vituo vya Arusha mjini, Mto wa Mbu na Engarasero ili kuweza kudhibiti hali hiyo na endapo gari halitakwua katika madaftari hayo kibali chake kitakwua ni batili na serikali itamfutia kibali cha kusafirisha abiria.

Akizungumzia suala la magari kutozwa ushuru zaidi ya mara moja Ndembeka alisema kuwa,vituo vilivyopo katika manispaa ya Arusha,wilaya ya Longido na Monduli katika eneo la Mto wa Mbu haviruhusiwi kutoza ushuru.

“Ni makosa kwa halmashauri yoyote ile kutoza ushuru,na ieleweke kwamba ushuru unatozwa mara moja katika kituo cha Eyasindito kilichopo wilayani Ngorongoro na si vinginevyo,” alionya Ndembeka.

Akizungumzia suala la huduma ya Mwasapila alisema kuwa, kuanzia sasa Mchungaji huyo atakuwa anatoa huduma siku ya Jumatatu mpaka jumamosi baada ya mchungaji huyo kuiomba Serikali kufanya hivyo.

“Kutokana na ombi la Mchungaji Mwasapila kwa serikali,kuwa siku ya jumapili anaomba iwe siku yake ya kuabudu na kupumzika hivyo katika vituo vyote nchini vibali vitakuwa vinatolewa kuanzia jumatatu hadi ijumaa ili kumpa fursa mchungaji huyo aweze kupumzika,” alisistiza ofisa huyo.

 Ndembeka aliongeza kuwa kufuatia hali ya barabara kwa sasa kuwa nzuri tofauti na kipindi cha nyuma magari 300-370 yamekuwa yakiwasili Samunge kila siku na wagonjwa kupata tiba ya “kikombe” na kuondoka.