Kamati Kuu ya Mazishi ya aliyekuwa msanii mashuhuri wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, imedai msanii huyo amefariki dunia akiwa maskini, kinyume kabisa cha umaarufu mkubwa aliokuwa nao wakati wa uhai wake.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtitu Gabriel, alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu makusanyo na matumizi ya fedha zilizotumika katika maombolezo, kuaga na mazishi ya Kanumba, aliyefariki dunia Aprili 7, mwaka huu na kuzikwa Aprili 10, mwaka huu.
Mbali na Mtitu kutoa ufafanuzi kuhusiana na fedha zilizokusanywa pamoja na matumizi yake, alikanusha taarifa za uvumi kuwa msanii huyo ameacha mali zenye thamani ya Sh. milioni 700.
“Hizi taarifa hazina ukweli ndani yake, ninachojua Kanumba amefariki akiwa na jina kubwa katika sanaa, lakini ni mtu mwenye pesa ya kawaida,” alisema Mtitu.
Alisema kinachozungumzwa na watu hakina ukweli.
Mjumbe wa Kamati hiyo, William Mtitu, alisema mali zilizoachwa na marehemu Kanumba ni magari matatu na, viwanja ambavyo hata hivyo, hakutaja idadi yake wala mahali viliko.
Kuhusu nyumba aliyokuwa akiishi eneo la Sinza, alisema kuwa ilikuwa ni ya kupanga.
Pia alisema alikuwa akimiliki kampuni inayohusika na uandaaji na utayarishaji wa filamu ijulikanayo kwa jina la “Kanumba The Great” jijini Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ambayo inamiliki studio, inaelezwa ina mchango mkubwa wa kuinua vipaji vya wasanii chipukizi, akiwamo Wema Sepetu na Elizabeth Michael, maarufu kama ‘Lulu’.
Hata hivyo, alikataa kueleza kiasi cha fedha alizoacha Kanumba na akaunti zake za benki kwa maelezo kwamba suala hilo ni la familia.
Awali, Gabriel Mtitu alisema wao kama kamati, walipokutana siku ya msiba wa nyota huyo wa filamu, kulikuwa hakuna kianzio chochote cha kufanikisha msiba.
Badala yake, alisema walifanya bidii ya kukusanya fedha ambazo zilitumika wakati wa msiba.
Mtitu alitaja makusanyo ya michango pamoja na matumizi ya fedha zilizotumika katika maombolezo hadi mazishi ya msanii huyo.
Alisema makusanyo ya michango yote ilikuwa ni Sh. 53,252,000 na kwamba, kati ya fedha hizo, zilizotumika ni Sh. 52,102,000.
Mtitu alisema fedha zilizotolewa ahadi ni Sh. 15,500,000, wakati ahadi ya vifaa ilikuwa ni Sh. 18,400,000. Alisema ahadi zilizolipwa ni Sh. 2,850,000.
Mtitu alisema gharama zote za maombolezo hadi mazishi zikiwemo taslimu na ahadi ni Sh. 70,502,000.
“Salio ni Sh. 4,000,000 ambazo zimekabidhiwa na zitaendelea kukabidhiwa kwa mama wa marehemu kadri ya marejesho ya ahadi yatakavyokuwa,” alisema Mtitu.
Alisema wao kama kamati wamekamilisha rasmi shughuli za msiba huo, na kuiachia familia iendelee na taratibu nyingine.
Mtitu alisema ili kuhakikisha wanamuenzi marehemu Kanumba, wanatarajia kuanzisha tuzo ya Steven ambayo itatoa changamoto kwa wasanii kuiga mfano wa utendaji wake wa kazi.
“Tuna mikakati ya kuanzisha tuzo ya Steven ambayo itatoa changamoto kwa wasanii kujituma ili waweze kufikia kiwango alichofikia katika uigizaji wake,” alisema Mtitu.
Akizungumzia malalamiko ya baadhi ya watu kutopewa nafasi ya kuuaga mwili wa marehemu, alisema ilishindikana kutokana na matarajio ya watu waliofika katika mazishi yake yalikuwa kinyume cha makadirio yao.
“Hatukutarajia idadi kubwa ya waombolezaji kujitokeza kiasi kile. Baada ya viongozi wa serikali kuondoka, kulitokea msongomano uliopelekea kamati kuzuiwa watu kuaga,” alisema Mtitu.
CHANZO: NIPASHE