Utajiri wa Lowassa Unavyoyatesa Makanisa Tanzania

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM)

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM)

Na Prudence Karugendo

KATIKA mafundisho ya Injili, ambayo ni maelezo kuhusu Yesu Kristo, inaelezwa kwamba mama mmoja alikamatwa na kupelekwa mbele ya Kristo akituhumiwa kufanya ukahaba huku wadau waliomkamata wakimtaka Kristo kutoa hukumu ili mama huyo aadhibiwe kulingana na maelekezo ya torati.

Kristo alitumia hekima yake na kusema sawa, anayejielewa ni msafi hajapata kutenda kosa la jinsi hiyo na awe wa kwanza kutoa adhabu husika. Kauli hiyo iliwafanya watu wote kutawanyika huku Kristo akimwambia mama yule aende zake na asirudie makosa yale.

Tunaona kwamba Kristo hakutumia njia yoyote kujinufaisha na udhaifu wa mwanamke huyo zaidi ya kutoa fundisho kwamba tunapohukumu ni lazima kwanza tujitazame sisi tuna usafi gani unaotuhalalisha kuwahukumu wengine. Hapa nchini kwetu kuna aina ya kashfa ambayo imetokea kufanana na makosa yanayotajwa kwenye torati kama makosa ya mauti, ufisadi.

Kama ilivyosemwa kwenye torati kwamba mzinzi anapaswa apigwe mawe mpaka afe, hata ufisadi unaonekana kuchukiwa kiasi cha kufananishwa na uzinzi kwenye torati, fisadi anatazamwa kwa jicho baya sana na Watanzania kwa sasa. Wapo watu wanafanya ufisadi na kujinufaisha nao lakini huku wakiunyanyapaa, hawataki kujiita wala kujulikana kwamba ni mafisadi.

La kushangaza ni kwamba ufisadi unaonekana ni mbaya, mchafu, watu hawautaki wala kuhusishwa nao, lakini hawakomi kuufanya! Kwa kuufanya ufisadi ni mtamu ila anayeufanya anaona aibu kuitwa fisadi! Mtu anayeitwa fisadi, hata kama anajielewa kuwa anaufanya ufisadi, tena kwa makusudi, na akielewa kwamba ananufaika nao, atapiga kelele kwamba anatukanwa, anaonewa wivu na mambo mengine ya kuipinga sifa hiyo ambayo kila mmoja wetu anaiona ni mbaya isiyofaa kwa mtu kutambulishwa nayo katika jamii.

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) jamii imemuweka wazi kuwa ni fisadi. Sitaki kumhukumu kwa vile sina ushahidi wa kutosha wa kunifanya nimuone hivyo. Ila nitasema kile ambacho jamii inakichukulia kama ukweli kumhusu. Lowassa ni mtumishi wa muda mrefu katika serikali na baadaye akawa Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu kwa kashfa ya kuipa zabuni ya ushindi kampuni ya kuzalisha umeme wa dhararua ya Richmond.

Wapo wanaomuandama Lowassa wakitaka asulubiwe kwa kashfa hiyo ya ufisadi sawa na mwanamke aliyepelekwa kwa Kristo akituhumiwa kwa ukahaba. Lakini hata hivyo wanaobeba tuhuma hizo dhidi ya Lowassa hakuna hata mmoja anayeweza kututhibitishia kwamba ni msafi asiyepata kutenda kosa kama lile analotuhumiwa nalo Lowassa.
Kwa hapo fundisho la Kristo ndipo linapochukua nafasi yake kwamba asiyepata kufanya au kuhusishwa na ufisadi na awe wa kwanza kumsulubu Lowassa. Ninalotaka kuliangalia katika makala haya ni namna Lowassa alivyoingia katika mbeleko ya kanisa na kanisa kumuwekea kinga, lakini kinga iliyo tofauti na ya Kristo kwa mwanamke aliyedaiwa ni kahaba.

Kristo aliposema kwamba anayejijua ni msafi na awe wa kwanza kurusha jiwe kutekeleza sheria ya torati ya kumpiga mawe mzinzi mpaka afe, alijikuta amebaki na yule mwanamke peke yake baada ya watu wote kutawanyika kwa aibu.
Kumbe watu wote walikuwa wakilitenda kosa lile. Baada ya hapo ndipo Kristo akamuasa mwanamke yule kutorudia makosa yake. Yule mwanamke akawa ameshinda kesi kwa njia ya aina yake.

Lakini linapokuja suala la kanisa na Lowassa tunaona kitu kilicho tofauti kabisa. Kanisa linapinga ufisadi, ila linajaribu kutumia mbinu kama aliyoitumia Kristo kumnusuru mama mzinzi. Pamoja na ukweli huo kanisa linashindwa kumwambia Lowassa nenda usirudie kutenda makosa haya.

Baada ya kutaka kumnusuru Lowassa kwa njia ya Kristo kwa mwanamke mzinzi Kanisa linang’ang’ani kubaki na Lowassa kwa manufaa yanayoonekana ni ya Kikanisa. Kanisa linaonekana kumweka Lowassa kwenye mbeleko yake na kuzunguka naye kila pahala, kitu kinachoonekana kama vile kanisa lina namna linavyojinufaisha na tuhuma zinazomkabili mtu huyo.

Katika nyakati tofauti tumeshuhudia kanisa likimualika Lowassa katika shughuli zake mbalimbali kana kwamba bila yeye kufika shughuli hizo haziwezi kupata baraka za Mungu! Ndiyo, tumeishapata somo kwamba kutuhumiana si kuzuri. Kristo alisema kwamba anayejua kwamba hajatenda kosa kama lile na awe wa kwanza kutoa adhabu husika. Lakini hata hivyo Kristo hakufundisha kwamba tunaweza kujinufaisha na tuhuma zinazomkabili mtu.

Kwahiyo kama kanisa linamuona Lowassa hana hatia basi lingemwambia nenda zako usirudie kufanya au kujihusisha na kashfa za aina hiyo na kisha kuachana naye. Lakini kitendo cha kanisa kuandamana na Lowassa karibu kila pahala likijinufaisha na michango na misaada anayolitolea kinatoa picha kwamba Lowassa anatiwa nguvu na kanisa ili aendelee kupata kwa njia anayotuhumiwa nayo huku akiwa amelindwa na kanisa. Kwa maana nyingine kanisa linamtia Lowassa ujasiri mpya ili kama ni ufisadi aendelee kuufanya kwa nguvu na kasi mpya!

Hakuna namna ambayo kanisa linaweza kusema kwamba linaupinga ufisadi ilhali likimtegemea mtuhumiwa wa ufisadi aliwezeshe kwa namna mbalimbali kwa kukitumia kile anachotuhumiwa nacho. Utasikia Lowassa kaalikwa katika kutunisha mfuko wa kanisa fulani, mara kaalikwa kwenye uzinduzi wa ujenzi wa kanisa, mara ujenzi wa kigango, kutiwa wakfu, uzinduzi wa kwaya nakadhalika. Na kote huko mwalikwa huyo anamwaga mapesa au ahadi.

Kwa nini kanisa halijiulizi mtu ambaye kwa muda wote wa maisha yake amekuwa mtumishi wa serikali fedha zote hizo anazipata wapi? Kwa nini hiyo isiwe njia ya kulifunua kanisa macho na kuanza kukiona kile ambacho mtu huyo anatuhumiwa nacho? Kwa njia hiyo tunawezaje kukosa kuamini kwamba katika fungamano la makanisa na Lowassa kuna kitu ambacho kimejificha ndani yake, kitu ambacho kinawezekana kuwa ni mpango wa nilinde nikulinde?

Kwa nini mtu ambaye anaandamwa na tuhuma za utajiri mchafu aonekane msafi kwa kanisa na kubebwa kila mahali akiwa amepewa kipaumbele? Kama nilivyoonyesha mwanzo kuhukumiana kwa tuhuma tu ambazo hazikuthibitishwa si jambo jema, hata Kristo alionyesha kutokubaliana nalo. Lakini vilevile kujinufaisha kwa kumkingia kifua mtuhumiwa nalo si jambo jema, sababu tunaona kwamba hata Kristo hakufanya hivyo.

Kwahiyo ingefaa kanisa litoe maelezo ya kwa nini lisihusishwe na ufisadi baada ya kuonekana linambeba mtu anayetuhumiwa kwa ufisadi na kumkingia kifua huku likiwa linajinufaisha naye kwa njia mbalimbali. Pamoja na hilo mtindo wa kanisa kutaka waamini wake watoe asilimia kubwa ya vipato vyao kwa kanisa bila kujali vyanzo vya vipato hivyo ni dosari kubwa kwa kanisa.

Kuna uwezekano mkubwa kanisa likajikuta linauchochea ufisadi, hata ujambazi, kwa kuvibariki vitu vilivyopatikana kwa njia hizo haramu baada ya vitu hivyo kutolewa kanisani kama sadaka takatifu. Mtazamo wangu ni kwamba kanisa lingetakiwa kujitenga na tamaa inayoweza kulifanya lionekane linashadidia uasi kwa kuwakumbatia tu watu wenye mali kana kwamba inatangazwa kwenye Injili kwamba wenye nacho ndio watakaoupata ufalme wa mbinguni.

Injili inatueleza wazi kuwa tajiri kufika mbinguni ni vigumu kuliko ngamia kupita kwenye tundu la sindano. Kwa kulizingatia hilo inabidi tujiulize kanisa linapata wapi ujasiri wa kuwakumbatia matajiri, ambao tayari wanaonyeshwa kwamba kuupata ufalme wa mbinguni ni kitu kigumu kwao, badala ya kuwashauri wakagawe mali zao
zote kwa masikini na kumfuata Kristo kama Kristo mwenyewe alivyomshauri Zakayo? Ikumbukwe Kristo hakumwambia Zakayo kwamba utajiri wako wote leta kwamgu.

Alimshauri akaugawe kwa masikini. Kwa mtazamo huo ningeweza kulielewa kanisa kama lingempa Lowassa ushauri wa kuachana na utajiri wake kwa kuwanufaisha maskini ili yeye apate kuokoka kuliko kanisa lenyewe kujinufaisha na utajiri huo wa Lowassa ambao ni kama unalinajisi hekalu hilo la Mungu.

prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512