Utafiti TAMWA waonesha vipigo kwa wanawake vimekithiri

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya akionesha ripoti hiyo kwa wanahabari

Mhariri Mkuu wa mtandao wa dev.kisakuzi.com (katikati) akiwa na waandishi wengine katika uzinduzi wa taarifa hiyo. Kulia ni Sam Maella wa ITV na Sanga wa Sanga wa The Citizen (kushoto)

Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), kimewataka viongozi wote ngazi ya wilaya kwa kushirikiana na wabunge kukemea vitendo vya unyanyasaji wa vipigo kwa wanawake nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya alipokuwa akizindua na kutoa ufafanuzi juu ya utafiti uliofanyika hivi karibuni mikoa mbalimbali nchini, ambao umebaini ongezeko la vipigo kwa wanawake.

Alisema katika ripoti ya utafiti huo mbali na kuibua masuala anuai ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia imeonesha kuwepo kwa idadi kubwa ya vipigo kwa wanawake vinavyofanywa na wanaume jambo ambalo linakwamisha juhudi za maendeleo ngazi ya familia.

Alisema idadi kubwa ya wanawake vijijini ni wazalishaji mali wazuri, hivyo endapo suala la vipigo litafumbiwa macho na Serikali kupitia viongozi wake juhudu za maendeleo katika jamii zitakwamishwa.

“Ukatili wa vipigo ni tatizo kubwa…na wote tunajua mtu anayepata kipigo kira mara hawezi kuwa mzalishaji mali mzuri, suala hili likifumbiwa macho umasikini mkubwa utaendelea kuzigubika familia zetu, hasa maeneo ya vijijini,” alisema Nkya katika ufafanuzi wake.

Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya alipokuwa akizindua ripoti ya utafiti


Aidha alisema katika utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano na waandishi kutoka vyombo anuai vya habari Tanzania, ukiwemo Mtandao wa dev.kisakuzi.com baadhi ya viongozi ngazi za Wilaya wameonekana kuwa vikwanzo katika utoaji wa taarifa hasa katika Wilaya za Tarime, Mvomero pamoja na Wilaya ya Kinondoni.

Ameongeza kuwa utafiti umebaini kuwepo kwa baadhi ya watendaji hasa wa vijiji kutofanya kazi zao ofisini jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi na kushindwa kutimiza wajibu wao.

Utafiti huo wa kihabari (journalistic survey) uliofanyika kuanzia mwezi Aprili 2012, TAMWA ulifanyika katika katika mikoa 20 ikiwepo 15 ya Tanzania Bara na mitano ya Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine uliangalia vitendo vya ukatili nchini. Vitendo vilivyolengwa ni ubakaji, vipigo kwa wanawake, kutelekeza wanawake na watoto, ukeketaji na kulazimisha watoto wa kike kulazimishwa kukatisha masomo na kuolewa.