Usu Mallya Awaasa Wananchi Kushiriki Kikamilifu Mchakato wa Katiba Mpya

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Usu Mallya(kushoto) akiwa na mwenyeji wake Diwani wa Kata ya Mkambarani, Daniel Shawa (CCM)

Hapa ngoma imenoga; Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Usu Mallya

Moja ya vikundi vya maigizo likitoa elimu kupitia sanaa hiyo

Na Mwandishi wa dev.kisakuzi.com Morogoro

MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uundwaji wa Katiba mpya ili itakapo kamilika sera na sheria za nchi ziendane na wananchi wake, jambo ambalo litasaidia kutatua migogoro anuai.

Mkurugenzi huyo aliyasema hayo jana eneo la Mkambarani mje kidogo ya Mji wa Morogoro ambapo linafanyika tamasha la Jinsia katika ngazi ya wilaya lililoandaliwa na TGNP, kuchochea juhudi za wananchi hasa waliopo pembezoni kushiriki katika mchakato wa maendeleo yao.

Baadhi ya wananchi kwenye mkutano huo


Akizungumza katika mkutano huo unaowashirikisha wanavijiji kutoka baadhi ya vijiji vya Mkoa wa Morogoro na baadhi ya mikoa ambao ni wanaharakati wa ngazi za jamii, alisema ushiriki wa wananchi ipasavyo katika mchakato huo itasaidia mabadiliko ya mfumo wa uandaaji wa sera na sheria ili zisiendelee kulalamikiwa na wananchi.

“Mfumo uliopo sasa yawezekana kabisa ukawa na upungufu, ndio maana hata kwa sasa baadhi ya maeneo yanapata huduma za kijamii huku maeneo mengine yakilegalega kihuduma,” alisema.
Alitolea mfano eneo la Mkambarani wananchi wanalalamikia migogoro ya ardhi hali hiyo inachangiwa na mfumo katika mgawanyiko wa rasilimali ikiwemo ardhi, ambapo baadhi ya makundi yamekuwa yakisahaulika huku wajanja wakineemeka na mifumo hiyo.
Alisema wananchi wanapaswa kushirikishwa kwa karibu katika uandaaji wa sera na sheria na pia kushirikishwa kwenye mipango ya maendeleo ili kuondoa mkanganyiko ambao hujitokeza hapo baadaye. “Wananchi lazima tushirikishwe katika mipango ya maendeleo…tukumbuke kwamba hakuna sera na sheria inayonihusu mimi bila mimi kushirikishwa,” alisema Mallya.

Aidha aliwataka wanawake na wapenda mabadiliko kushiriki katika vuguvugu la kupambana na mfumo dume na kandamizi ambao kwa kiasi kikubwa unawaathiri akina mama. “Tukubali kuwa huu ni mchakato wa mabadiliko, tukatae uonevu na kupambana na mifumo yote kandamizi kwa kutumia umoja wetu pamoja na ushirikiano…umefika wakati wa kushirikiana katika masuala ya maendeleo, tusiishie kwenye harusi na misiba tu,” aliongeza.

Tamasha la jinsia ngazi ya wilaya linalofanyika nje kidogo ya mji wa morogoro linatarajiwa kumalizika leo jioni ambapo washiriki kwa pamoja watatoka na maadhimio ambayo yatafanyiwa kazi kulingana na maitaji.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com