Na Rajab Mkasaba, Zanzibar
OFISI ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imeeleza kuwa maelekezo na ushauri unaotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa watendaji kila mara, umeongeza ari ya utendaji na ufanisi wa kazi.
Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi uliyasema hayo katika kikao maalum na Rais Shein katika muendelezo wa kukutana na uongozi wa Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia mpango kazi wa Wizara na uhusiano wa MKUZA na Dira ya 2020.
Katika Kikao hicho Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee walishiriki, kikao ambacho kilifanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Ukieleza mikakati iliyojiwekea, ofisi hiyo ikiwemo ile ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2011/12, ukiongozwa na Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Haji Omar Kheir ulipongeza hatua anazochukuwa Dk. Shein katika kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi kupitia Ilani ya CCM zinatekelezwa kikamilifu.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa utaratibu aliojipangia wa kukutana na watendaji wakuu wa Wizara mbali mbali umeweza kusaidiaa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha utekelezaji huo wa ahadi unatekelezwa kwa vitendo.
Katika utekelezaji wake wa MKUZA, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ilieleza kuwa inatekeleza mipango yake ambayo inahusisha Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo Shamba la Kilimo cha Mbogamboga Bambi na Ujenzi wa Hospitali ya KMKM na mengienyo.
Ofisi hiyo ilieleza malengo yake ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2011-2011 ambapo vipaumbele zaidi vimewekwa katika kuendeleza Umoja wa Kitaifa na mashirikiano pamoja na lengo la kuimarisha uwezo na utoaji wa huduma ikiwemo usafishaji wa miji na uendeshaji wa Serikali za Mitaa, Wilaya na Mikoa na kuimarisha pamoja na kuongeza uwezo wa Idara Maalum za SMZ.
Pia, ilieleza kuwa tayari viongozi wa Mikoa na Wilaya wameanza kuelimisha wananchi mipango ya serikali kwa kutumia vyombo vya habari kwa lengo la kuwasaidia kufahamu mambo na mipango ambayo serikali yao inatekeleza kwa ajili yao na kueleza juhudi walizozichukua katika kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yenye mizozo.
Aidha, Ofisi ilieleza kuwa ina lengo la kuimarisha mfungamano wa Kikanda ili Wazanzibari waweze kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na Jumuiya ya Afrika Mashariki,Jumuiya ya Kusini mwa Afrika na Jumuiya nyengiene za Kikanda.
Lengo jengine ni pamoja na kuwashajihisha Wazanzibari wanaoishi nchi za nje katika kushiriki na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ambapo kwa mujibu wa uongozi huo tayari Wazanzibari hao wameanza kuchangia katika sekta za kijamii ikiwemo elimu na afya katika maeneo ya Unguja Ukuu, Makunduchi,.Vuga na Skuli ya Miti Ulaya Wete Pemba
Kwa upande wa Baraza la Manispaa Ofi hiyo ilieleza juhudi zake ilizozichukua katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la kuzagaa kwa ngombe na wanyama wengine wanaozurura ovyo katika maeneo ya mjini wa Zanzibar ambapo jumla ya wanyama 69 wamekamatwa wakiwemo ngombe 44, punda 13 na mbuzi 12 na wachungaji wao kulipizwa faini.
Baraza la Manispaa limesimamisha utoaji wa leseni zote za gereji ndani ya Mji Mkongwe na limeishauri Idara ya Upimaji Ardhi kutenga maeneo maalum ya shughuli za gereji ambapo tayari hatua ya kutoa notisi kwa wenye gereji Mji Mkongwe imechukuliwa.
Pamoja na hayo, Wizara ilieleza kuwa kiwanja cha MnaziMmoja kimeingizwa katika Mradi wa Mpango wa Kuimarisha huduma za miji ya Zanzibar (ZUSP) ambao utajenga mtaro mpya wa chini kwa chini kwa ajili ya kutoa maji kwenye kiwanja hicho.
Pia, kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini, Ofisi ilileleza lengo lake la kushirikiana na Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kufanya utafiti juu ya kero ya unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji.
Sambamba na hayo, Ofisi ya Rais, ilieleza kuwa tayari Wizara ya Kilimo na Maliasili chini ya kitengo cha Umwangiliaji maji tayari wamefika katika bonde la Ukele Kaskazini Pemba na kukagua uwezekano wa kuzuia maji chumvi yasiingie katika bonde la mpunga.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi hiyo kwa juhudi zake inazozichukua na kueleza kueleza kuwa mkutano huo utawasaidia zaidi viongozi hao kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi ili kufikia malengo yaliowekwa yakiwemo ya robo ya kwanza ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.
Dk. Shein aalieleza matumaini yake makubwa ya mradi wa Benki ya Dunia utakaoanza hivi karibuni ambao utasaidia kuendeleza mji wa Zanzibar na kupongeza hatua za usafi zinazochukuliwa na Manispaa na kutaka kuongezwa juhudi zaidi katika suala zima la usafi wa mji.
Aidha, Dk. Shein ameleza kuwa tayari ZSTC imeandaa taratibu za kuwakopesha fedha wanunuzi wa karafuu kwa ajili ya shughuli zao ambapo milioni 200 zimetengwa ambapo utaratibu utawekwa katika kuzirejesha fedha hizo kupitia mkataba maalum.
Nae Maalim Seif Sharif alieleza haja ya kuajiri wahudumu katika vituo vya afya ambao wanaishi karibu na vituo hivyo ili kurahisisha utoaji huduma hiyo kwa wananchi.
Aidha, aliueleza uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kuendeleza juhudi za kupambana na vita vya wauzaji wa karafuu kwa magendo ambao hivi sasa wamekuwa wakitumia njia zisizopitika kwa usafiri wa aina yoyote, ambapo serikali imeahidi kuzitafutia ufumbuzi wa haraka njia hizo ili kuendelea kuliokoa zao hilo.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee akitoa mchango wake katika kikao hicho alieleza kuwa ipo haja ya kuwekwa adhabu kali kwa wanaotupa taka ovyo mjini kwani baadhi ya miji katika Bara hili la Afrika imepiga hatua katika suala la usafi ukiwemo mjini mkuu wa Rwanda, Kigali.