Usalama wa Taifa wapinga kumdhuru Dk Stephen Ulimboka

Dk Stephen Ulimboka akiwa chumba cha wagonjwa mahututi Muhimbili

IDARA ya Usalama wa Taifa wa Tanzania imepinga kuhusika kwenye tuhuma zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa inahusika na sakata la kutekwa, kuteshwa na hatimaye kujeruhiwa vibaya kabla ya kutupwa msituni kwa kiongozi wa madaktari nchini Stephen Ulimboka
Kwa mujibu wa taarifa yake kwa vyombo vya habari idara hiyo imesema; “katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza taarifa zenye tuhuma kadhaa dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa. Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari zikiihusisha Idara hii na matukio ambayo yanaidhalilisha na kuzua maswali mengi kwa wananchi.”
“Kati ya tuhuma hizo ni tukio la kutekwa kwa Dk. STEPHEN ULIMBOKA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari na madai ya kufanywa kwa mipango ya kuwadhuru baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Upinzani. Gazeti moja la kila wiki limekuwa likurudia tuhuma hizo mara kwa mara kwa madai kwamba ni habari za uchunguzi na kuihusisha Idara”.
Taarifa hiyo imesema taarifa zinazotolewa dhidi yake ni UZUSHI na UONGO ambazo zina nia ya kuharibu jina na sifa ya Idara. Taarifa hizo zimekuwa zikiunganishaunganisha vipande vya taarifa mbalimbali ili kukidhi malengo yaliyokusudiwa na wanaolitumia gazeti hilo. Idara haikuhusika wala haihusiki na matukio yoyote yaliyotajwa katika tuhuma hizo.
“Hivyo tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo. Matukio yaliyotajwa katika tuhuma hizo yanachunguzwa na Jeshi la Polisi ambacho ndicho Chombo Chenye Dhamana, na kwa Maslahi ya Taifa si vizuri kuachia upotoshaji huo uendelee.”
“…tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa uzushi na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Idara hazitatuvunja moyo bali zitatuunganisha na hivyo kutuimarisha katika azma yetu ya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kubaki salama kwa kushirikiana na wanachi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.” Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.