Na Anne Kiruku, EANA, Arusha
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki (IUCEA) Prof. Mayunga Nkuya alisema mjini Nairobi, Kenya kwamba Kanda ya Afrika Mashariki imefikia asilimia nne tu ya usajili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu ikiwa imeshuka kutoka asilimia tano za miaka iliyopita.
“Kwa kweli, usajili hivi sasa unashuka,” alisema Prof Nkunya, huku akifafanua kwamba kanda hiyo ina idadi ndogo zaidi ya usajili wa wanafunzi katika elimu ya juu kwenye kanda nzima ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hayo yalijitokeza jana wakati Prof Nkunya alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi juu ya maandalizi ya mkutano wa pili wa Jukwaa la Wasomi na Sekta Binafsi (APS) kufanyika mjini humo kati Oktoba 24 na 26, 2013.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuunganisha wasomi na Sekta Binafsi kwa kushirikisha Sekta ya Umma”. Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe wapatao 250 wakiwemo wasomi, taasisi na sekta binafsi. Prof Nkuya alipendekeza usajili wa wanafunzi nyuo vikuu ufikie asilimia 40 na kuongeza kuwa usajili wa wananfunzi katika kanda hiyo kwa ngazi hiyo ya elimu uko chini mno ya kiawango kinachotakiwa.
Alieleza pia kwamba kanda hiyo inahitaji vyuo zaidi vya elimu ya juu kuhakikisha kwamba wanafunzi wengi wanapata nafasi ya kuwawezesha kujipatia elimua ya juu.
Changamoto zinazotokana na upanuzi wa elimu ya juu alisema hazina budi kushughulikiwa ipasavyo lakini alionya kuwa hatua hiyo isiwe kikwazo cha kuzuia upanuzu wa elimu ya vyuo vikuu. Moja ya matatizo yanaikabili sekta ya elimu ya juu kwa mujibu wa Prof Nkunya ni ugoigoi wa kufanya mabadiliko katika mfumo wa elimu katika vyuo vikuu vya kanda hiyo ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu ya juu katika Afrika mashariki. Mkutano wa kwanza wa aina hiyo ulifanyika, Arusha, Tanzania mwaka jana.