Usajili mashindano ya Klabu CAF

Nembo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)

*FIFA yamteua Minja kusimamia mechi

SHUGHULI ya usajili kwa ajili ya timu za Tanzania zitakazoshiriki michuano ya ngazi ya klabu Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) inaendelea.

Yanga itacheza Ligi ya Mabingwa (CL) wakati Simba itashindana katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CC). Kwa upande wa Yanga hadi sasa imeshawasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) majina ya wachezaji 28 wakati Simba majina 24 kwa ajili ya usajili huo.

Mwisho wa kufanya usajili ni Desemba 31 mwaka huu, na kila klabu inaruhusiwa kusajili hadi wachezaji 30. Hata hivyo Agosti mwakani kutakuwa na usajili wa dirisha dogo kwa timu ambazo hazikumaliza nafasi zote 30.

Kuna mifumo miwili ya usajili; online (mfumo wa mtandao) au offline (kutuma fomu za usajili CAF kwa njia ya DHL). TFF tumeamua kutumia mfumo wa online.

Wakati huo huo, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Katibu wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Joan Minja kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia kati ya Zambia na Botswana.

Mechi hiyo ya raundi ya awali kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Wasichana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Azerbaijan itachezwa kati ya Februari 3, 4 au 5 mwakani jijini Lusaka.

Kwa upande wa Afrika nchi ambazo zitacheza raundi ya awali ya michuano hiyo ni Afrika Kusini, Botswana, Cameroon, Gambia, Ghana, Guinea, Namibia, Nigeria, Sierra Leone, Tunisia na Zambia.