HAYO yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki Ofisini kwake katika mkutano wake na waandishi wa habari. Amesema katika taarifa yake aliyoisoma kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mohamed Gharib Bilal katika ziara yake ya siku moja katika Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 21/07/2013 katika ukumbi wa Karimjee alisisitiza kuwa zoezi la usafi wa Jiji la Dar es Salaam ni endelevu mpaka tutakapofika wakati wa kuridhisha kuwa JIJI LETU SASA NI SAFI.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesisitiza kuwa jukumu hili la usafi katika Jiji letu hili litafanikiwa ikiwa mambo makubwa matatu yatazingatiwa:
1.Ushiriki wa Wakazi wa Dar es Salaam (Wana Dar es Salaam) kikamilifu katika kufanikisha zoezi hili.Hii inaonekana kuwa kama wakazi wa Dar es Salaam tutakuwa na utamaduni wa kupenda usafi na kuchukia uchafu basi tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani sisi tutakuwa askari wa sisi kwa sisi. Hata hivyo ikitokea umemuona mwenzako amepanga biashara sehemu isiyotakiwa au ametupa takataka ovyo tutakuwa wa kwanza kukemeana sisi kwa sisi na kuacha kufanya hivyo sambamba na kuacha kununua bidhaa hizo katika maeneo yasiyofaa.
2.Viongozi/Wanasiasa kukemea suala hili la uchafu katika Jiji la Dar es Salaam: Hii imeonekana kuwa Jitihada, Juhudi na Nguvu nyingi zimekua zikifanywa na Serikali yetu ili kuhakikisha Jiji letu linakua safi,lakini kwa bahati mbaya imeripotiwa/imeonekana kuwa kuna viongozi/Wanasiasa wengine wametumika katika kuwapa viburi baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kufanya biashara katika maeneo yasiyotakiwa hivyo kusababisha hasara ya kutupa takataka ovyo na kukwepa kulipa ushuru wa bidhaa wanazoziuza ili hali wamepangiwa maeneo yao husika kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
3.Wanahabari/Waandishi wa Habari: Jukumu la waandishi wa habari ni kubwa sana katika kufanikisha kampeni hii kwani wao ndio wamekuwa wakitupatia habari mbalimbali za kuhusu uchafu wa Jiji la Dar es Salaam hivyo ninawaomba kuendelea kushirikiana katika kuibua sehemu ambazo zimekaidi katika kufanikisha zoezi hili na kuziripoti/kukemea na kuelimisha moja kwa moja kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari ili Jamii kwa ujumla ipate kujua hali ilivyo na kuacha tabia hiyo.
WITO
umetolewa kwa wakazi wa Dar es Salaam tujenge utamaduni wa kuchukia uchafu na kulitunza na kulilinda Jiji letu la Dar es Salaam,aidha wamachinga wafanye biashara zao katika maeneo yao waliyotengewa ili kuepusha uchafuzi wa mazingira pamoja na usumbufu wa hapa na pale na sheria na taratibu zitachukuliwa kwa yeyote atakaesababisha uchafu katika Jiji letu la Dar es Salaam.
TUKIAMUA TUNAWEZA KWA PAMOJA TUSHIRIKIANE KATIKA KUWEKA MAZINGIRA YA JIJI LA DAR ES SALAAM KUWA SAFI.