URA Wafalme Wapya Mapinduzi Cup 2016

URA-bingwa

Timu ya URA ya Uganda imetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2016 kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro usiku wa jana katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Ushindi huo ambao unakwenda sambamba na kitita cha Sh. Milioni 10, unaifanya URA iwe timu ya pili ya Uganda kutwaa taji hilo, baada ya KCCA mwaka juzi.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nassor, hadi mapumziko, URA walikuwa mbele kwa bao 1-0.Bao hilo lilifungwa na Julius Ntambi kwa kichwa, akimalizia krosi ya Villa Oromchani kutoka upande wa kushoto.

URA walikaribia kupata bao la pili dakika ya 37 baada ya Elkannah Nkugwa kupiga nje na kupoteza pasi ya Moor Semakula. Kwa ujumla, URA ilitawala mchezo na kuishika Mtibwa Sugar, ambayo safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Hussein Javu anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC, iliishindwa kupasua ukuta wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda.

Kipindi cha pili, Mtibwa Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mecky Mexime ilijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la kusawazisha, lakini wakasahau kuongeza umakini wa kujilinda, hivyo kuwapa fursa URA kupata mabao mawili zaidi.

Mtibwa-fainali-4

Peter Lwasa aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Villa Oromchani, aliifungia URA mabao mawili ndani ya dakika tatu – kwanza dakika ya 85 baada ya kuunasa mpira uliopigwa fyongo na beki Dickson Daud na lingine dakika ya 88 akimalizia pasi ya Julius Ntambi.

Jaffar Salum aliyeingia kuchukua nafasi ya Hussein Javu mwishoni mwa kipindi cha pili, aliifungia bao la kufutia machozi Mtibwa Sugar dakika ya 90, baada ya kumlamba chenga Jimmy Kulaba.

Pamoja na kutwaa ubingwa, URA pia imetoa mfungaji bora, ambaye ni Peter Lwasa aliyemaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Villa Oramchani wa URA pia, mabao mawili sawa na Awadh Juma wa Simba SC, Donald Ngoma wa Yanga SC, Mohammed Abdallah wa JKU na Kipre Tchetche wa Azam FC. Mtibwa Sugar wamepatiwa Sh. Milioni 5 kwa kushika nafasi ya pili.

ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI
Mwaka Bingwa Mshindi wa Pili
2007 Yanga SC Mtibwa Sugar
2008 Simba SC Mtibwa Sugar
2009 Miembeni KMKM
2010 Mtibwa Sugar Ocean View
2011 Simba SC Yanga SC
2012 Azam FC Simba SC
2013 Azam FC Tusker FC
2014 KCCA Simba SC
2015 Simba SC Mtibwa Sugar
2016 URA Mtibwa Sugar