Dodoma
KAMBI ya Upinzani Bungeni, imeunga mkono juhudi za Serikali za kupinga nia ya, Kampuni ya BAE systems ya Uingereza ya kutaka kulipa fedha za Rada sh. bilioni 75.2 za Tanzania kupitia kwa Asasi zisizo za kiserikali za Uingereza.
Pia imeitaka kampuni hiyo ya BAE systems kulipa fedha hizo haraka iwezekanavyo, na kutaka wahusika wote wa kashfa ya rada, akiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria kwa kufikishwa mahakamani.
Imesema kuwa iwapo watuhumiwa hao hawatachukuliwa hatua, ni dhahiri kuwa taifa haliwezi kuwa na uhakika wa kuzilinda vizuri fedha hizo za rada pindi zikilipwa, pamoja na fedha nyingine za umma ambazo zinaweza kuendelea kupotea kwa sababu umekuwa ni utamaduni wa Serikali kutochukua hatua.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Susan Lyimo alisema hatua hiyo itakuwa ni uzalilishaji mkubwa kwa watanzania wote.
Kambi hiyo pia imepinga fedha za rada kulipwa Serikali kwa kuwa haiaminiki, na kuongeza kuwa “ikitiliwa maanani kuwa fedha hizo zilizopotea mikononi mwa Serikali hii iliyopo madarakani na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na serikali kuwawajibisha wahusika wa upotevu huu.
“Na hata wakati kesi hiyo ikiwa mahakamani serikali yetu haikuomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo ila leo wako mstari wa mbele kudai fedha, hivyo tunaliomba Bunge liazimie kuanzishwa kwa Akaunti ya muda ya fedha za Rada.
…Akaunti hiyo itasimamiwa kwa pamoja na, wawakilishi wa Asasi zisizo za kiserikali za Tanzania , wawakilishi wa sekta binafsi na wawakilishi wa Serikali,” alisema Lyimo.
Pia akalitaka Bunge lijadili na kuamua kipaumbele cha matumizi ya fedha hizo chini ya usimamizi wa akaunti hiyo, kwa kuzingatia zaidi maslahi ya wengi kadri fedha hizo zitakavyoonekana kutosha.
“Aidha, azimio hilo limpe mamlaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua matumizi ya fedha hizo kama anavyofanya kwa fedha nyingine za umma.
Akizungumzia kuhusu viongozi wa Serikali kuishi hotelini, Msemaji huyo wa Kambi ya Upinzani aliitaka Serikali kujieleza kwanini ilitumia mabilioni ya fedha za walipa kodi kujenga nyumba za kuishi watumishi wa serikali lakini baadaye ikaziuza.
“Mheshimiwa Spika, wakati nyumba za Serikali zilijengwa na kuuzwa, baadhi ya mawaziri wanakaa hotelini. Kwa siku gharama ya hoteli hizo ni kati ya sh. Laki tano na sita, tukipiga hesabu ya kiongozi mmoja aliyekaa hotelini kwa miezi saba tangu aapishwe, ni dhahiri jumla ya sh. Milioni 110.2 zitakuwa zimetumika.
…Je, ni viongozi wangapi wanakaa hotelini na mpaka sasa wameliingizia taifa hasara kiasi gani na je, serikali imechukua hatua gani dhidi ya viongozi waliouza nyumba hizo? alihoji Lyimo.
Akiendelea kuzungumza, Msemaji huyo wa Kambi ya Upinzani alisema majukumu ya Sekretariati ya maadili ni mengi na yanalenga kuhakikisha kuwa tabia na mienendo ya viongozi wa umma inazingatia misingi ya maadili na maadili yaliyoainishwa katika sheria namba 13 ya mwaka 1995.
Hivyo ikapendekeza mchakato wa Katiba mpya uzingatie pia jinsi ya kuiondoa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma chini ya Ofisi ya Rais, ili iwe taasisi huru na iwajibike moja kwa moja kwa Bunge.
Kambi hiyo pia imesikitishwa na kitendo cha Sekretariati ya Maadili ya Umma kuomba posho za vikao na kuongeza kuwa “tulitarajia kuwa sekretariati ya maadili ya utumishi wa umma ingekuwa ni mfano katika suala la posho za vikao, lakini kwa bahati mbaya nayo inaomba sh. Milioni 28.6 kwa ajili ya kulipia posho katika vikao mbalimbali vya ofisi.
…Jambo hili halikubaliki kabisa na ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wa nchi hii, maadili ni jambo la msingi sana na ofisi hii ndiyo kinara wa uratibu wa maadili katika nchi yetu, lakini kinachosikitisha Idara ya Ukuzaji wa maadili imetengewa sh. 44, 280, 000 tu, kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa kampeni katika Wilaya na Mikoa.
…Tukipiga hesabu kwa wilaya 133 nchini, ni dhahiri kuwa kila wilaya itakuwa imetengewa sh. 332, 932 tu, kwa ajili ya shughuli za kuelimisha maadili kwa watumishi wa umma,” alisema.