Upinzani waiponda bajeti, wasema imejaa upotoshaji

Baadhi ya wabunge waliotoa maoni yao kuhusiana na bajeti hiyo, walieleza kwamba ni bajeti yenye lugha ya kufurahisha na kugusa hisia za watu, ya kinadharia lakini isiyo na ubunifu.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema: “Mkulo ametoa maelezo ya kisiasa…serikali imewapiga wafanyakazi changa la macho kwa sababu haijaeleza itapunguza kodi kwenye mishahara kwa asilimia ngapi na wala hata haijasema kubana matumizi yasiyo ya lazima itaokoa asilimia ngapi ya mapato yake na zitakwenda wapi.”

Alisema bajeti ya kambi yake, itaainisha kila senti itakayopatikana kutokana na kubana matumizi na namna itakavyotumika.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, alisema “hii ni bajeti ya kulipa madeni, serikali imetenga Sh. 1.9 trilioni sawa na asilimia 13 ya bajeti kwa ajili ya kulipa madeni.”

Alisema bajeti hiyo pia imechukua sehemu ya mapendekezo ya bajeti ya upinzani ikiwemo punguzo la tozo za kodi ya mafuta na kupunguza posho.

Alifafanua kwamba awali, Waziri Mkulo aliahidi nishati ingekuwa kipaumbele, lakini inashangaza miundombinu kutengewa kiasi kikubwa cha fedha. Aliongeza: “Kiasi kilichotengwa kwenye nishati kinaweza tu kukamilisha mradi mmoja kati ya mingi iliyopo.”

Mbunge wa Bariadi Magharibi (UDP), John Cheyo, alisema inashangaza bajeti kuendelea kutegemea wafadhili ambao wakati mwingine hawatekelezi ahadi zao. “Ni asilimia 50 tu ya ahadi ya fedha zilizoahidiwa na wafadhili mwaka jana zilichangiwa kwenye bajeti hiyo.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, alisema “bajeti inamwelekeo wa kupunguza ukali wa maisha.”

Serukamba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, alisema kuwa amefurahi kwa serikali kuipa miundombinu kipaumbele cha kwanza kwa kuwa hayo yalikuwa mapendekezo ya kamati yake.

Mbunge wa Bumbuli (CCM) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, alisema bajeti ni nzuri, lakini kiasi cha fedha kilichotengwa kwenye sekta ya nishati ni kidogo ikilinganishwa na idadi ya miradi inayokusudiwa kutekelezwa.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema: “Ni bajeti ya propaganda…bajeti inazungumza kuzalisha megawati 260 ambazo ni pungufu kwenye Gridi ya Taifa, hapo ni sawa na kuwa hakuna ongezeko lolote la uzalishaji wa umeme kulingana na mahitaji.”

Alisema bajeti imeshindwa kutatua kilio cha wafanyakazi wanaotaka kupunguziwa kodi kwenye mishahara “kwa bajeti hii, wafanyakazi wanaendelea kuishi kwa matumaini.”

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema inashangaza kuona serikali ikiendelea kuwapigia magoti wafadhili na kutangaza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima wakati imetenga sh. trilioni tatu kwa ajili ya posho na matumizi mengineyo.

“Serikali kusema inapunguza matumizi yasiyo ya lazima ni kuwaridhisha tu watu kwa sababu imetenga fungu kubwa la matumizi hayo,” alisema Kafulila.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya, alisema “inafurahisha kwa serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima lakini inasikitisha kwa sababu bado tunaendelea kutegemea wafadhili…ni wakati sasa wa kuweka msisitizo kwenye ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato.”

WAKAZI DAR WAIKOSOA

Wakazi kadhaa wa Jiji la Dar es Salaam wametoa maoni yao kuhusu bajeti ya serikali yamwaka 2011/12 iliyosomwa jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Mathias Kipara, alisema bajeti hiyo haijakidhi haja na matakwa ya wananchi.

“Ugumu wa maisha utaendelea kuwepo kwa sababu matatizo yanayomkabili Mtanzania yameguswaguswa tu, tulitarajia bajeti hii ingegusa matatizo sugu kama mgao wa umeme badala yake imekuwa ya kuisindikiza ile iliyopita,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo, matarajio ya Watanzania hivi sasa ni kuendelea kuvutana na serikali yao.

“Kwa upande wa elimu tulitegemea serikali ingetenga fedha ya kutosha, lakini ile iliyotengwa haiendani na mahitaji yaliyopo kwenye sekta hii, wanafunzi ni wengi wanaotegemea mikopo, lakini fedha hazitoshi,” alisema.

Pia alisema bajeti hiyo haijaonyesha ukusanyaji wa mapato ya serikali badala yake imeongeza kodi inayowabana wananchi.

“Tulitegemea kodi iongezwe kwenye maeneo kama madini, lakini kila mwaka imekuwa ikilenga vinywaji na sigara kama ndio muhimili wa ukusanyaji wa mapato, tulitegemea mishahara ya wabunge ingekuwa kama ya wafanyakazi wa umma,” alisema.

Waziri wa Mikopo wa Daruso, Joseph Sylvanus, alisema wamefarijika kwa upande mmoja wa serikali kukubali kupunguza gharama za safari na miradi isiyo na tija.

Dereva wa daladala, Deus Mosha, alisema kuwa, kitendo cha serikali kuongeza faini kwa baadhi ya magari yanayofanya makosa mbalimbali kutoka Sh. 20,000 hadi 50,000 kumelenga kuikandamiza zaidi sekta hiyo.

“Kwa mfano, spea (vipuri) vya magari kwa sasa bei zake zipo juu, mishahara hatulipwi na wamiliki wetu wa magari, halafu tunatakiwa kila siku kupeleka Sh. 35,000,” alisema na kuongeza: “Bado serikali leo hii inatutaka tulipe faini ya Sh. 50,000 si wanataka tuwe majambazi.”

“Jamani serikali inaonyesha wazi kuwa imelenga kutunyima ugali na familia zetu kuendelea kuwa masikini, tunakoelekea ni wapi?” alihoji.

Hata hivyo, NIPASHE ilishuhudia baadhi ya maeneo wananchi wakiwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na wengine walipohojiwa walisema kuwa bajeti hiyo haiwahusu kwa kuwa ni ya wabunge na watu wanaopokea mishahara mikubwa.

Imeandikwa na Joseph Mwendapola na Sharon Sauwa, Dodoma na Romana Mallya na Erick Mashafi, Dar.

source:Nipashe