Upinzani Ghana Wamsusia Rais Mahama

CHAMA rasmi cha upinzani nchini Ghana, kimesusia sherehe za kuapishwa kwa rais mpya John Mahama kufuatia uchaguzi wa mwezi jana uliokumbwa na utata.
Chama cha New Patriotic Party (NPP) kilisema kuwa bwana Mahama hakushinda uchaguzi huo kihalali.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo, yalionyesha bwana Mahama akiwa na aslimia 50.7 idadi ambayo inatosha kuweza kuzuia duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya mpinzani wake Nana Akufo-Addo, aliyepata asilimia 47.7 ya kura.
Kabla ya kuapishwa kwake, bwana Mahama alitoa wito wa amani na umoja nchini Ghana, nchi ambayo inaonekana kama mfano mzuri wa demokrasia barani Afrika.
Bwana Mahama alikuwa makamu wa rais wa Ghana hadi pale kifo cha ghafla cha aliyekuwa rais,John Atta Mills kutokea mwezi Julai.
Tangu hapo alihudumu kama rais wa mpito.
Katika hotuba yake, rais Mahama aliwaambia wananchi wa Ghana kuwa hatawaangusha .
Akiwa amevalia gauni nyeupe iliyorembeshwa kwa rangi za bendera ya nchi hiyo,rais John Mahama alitoa kauli ya upatanishi mbele ya umati mkubwa wa watu waliofika kumshangilia.
Madai ya ulaghai na wizi wa kura, bila shaka yataathiri sifa yake kwa muda.
Lakini kuwepo kwa baadhi ya marais wa Afrika katika sherehe ya kuapishwa kwake, kunaonyesha kuwa bwana
Mahama anaungwa mkono na jamii ya kimataifa.

-BBC