Na Janeth Mushi, Arusha
TATIZO la upatikanaji wa mafuta bado limeendelea kuwa kero katika maeneo mengi jijini hapa kutokana na vituo kadhaa vinavyouza mafuta ya dizeli na petroli kufungwa kwa madai kuwa havina mafuta.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa Thehabari mjini hapa katika maeneo mengi jana, ulishughudia kuwepo kwa foleni kubwa za magari yaliyokuwa yakisubiri mafuta hayo.
Katika kituo vya Mt. Meru kilichopo eneo la Philips barabara Kuu ya Arusha-Moshi na katika vituo vingine vya kampuni hiyo vilivyopo maeneo ya Mabuda barabra iendayo Wilaya ya Monduli, kumekuwa na msongamano mkubwa.
Vituo vingine vingi vikiwemo vya BP, kile cha Manjis kilichopo barabara ya Sokoine, kituo cha Oryx kilichopo eneo la Clock Tower na Njake kilichopo mtaa wa Goilondoi na kituo cha Engen, kilichopo barabara kuu ya Arusha-Moshi vyote vilikuwa vimefungwa kwa kukosa bidhaa hiyo.
Mfanyakazi mmoja wa kituo cha Manjis ambaye hakutaka jina lake kuchapishwa gazetini alidai kuwa wanatarajia kupata mafuta siku ya Jumatatu ijayo huku kituo cha Oryx kikidai kinatarajia kupata mafuta leo.