RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Januari 10, 2013, amekamilisha ziara yake yenye mafanikio makubwa katika Mkoa wa Tabora kwa kuweka jiwe la msingi la Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora.
Katika kitendo chake cha kuhitimisha ziara yake ya siku tano Mkoani humo, Rais Kikwete ameungana na mamia ya wananchi wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kwenye sherehe za kuweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja huo unaogharimiwa na Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania.
Uwanja wa Tabora ni moja ya viwanja vitatu vya ndege ambavyo vinatengenezwa upya na kupanuliwa katika Mradi unaogharimu Sh. Bilioni 45 zilizotolewa na Benki ya Dunia na Sh. Bilioni tisa zilizotolewa na Serikali ya Tanzania. Mbali ya Tabora, viwanja vingine kwenye Mradi huo ni Uwanja wa Ndege wa Bukoba na Uwanja wa Ndege wa Kigoma.
Akizungumza kwenye sherehe hizo, Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa mbali na mkopo huo wa Benki ya Dunia, Wizara yake pia inaendesha Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Sumbawanga na Shinyanga na uwekaji taa za kuongozea ndege kwenye Uwanja wa Tabora. Mradi huo unagharimiwa kwa mkopo wa Sh. Bilioni 100 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – European Investment Bank.
Uwanja wa Tabora unakaratabiwa na kupanuliwa kwa awamu tatu. Katika awamu ya kwanza itajengwa njia ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami kwa urefu wa mita 1,900 na upana wa mita 30. Hii itawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 70 kutua kwenye Uwanja huo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bwana Omar Chambo amemwambia Rais Kikwete kuwa katika awamu ya pili, litajengwa eneo la maegesho ya ndege lenye uwezo wa kuegesha ndege tatu kwa wakati mmoja na kujenga kwa jengo la kisasa la abiria na mizigo pamoja na kujenga kiungio (taxiway).
Amesema kuwa katika awamu ya tatu itajengwa njia ya pili ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali imepanga kujenga kituo kikubwa cha hali ya hewa ambacho kitakuwa moja ya vituo vikubwa zaidi vya hali ya hewa katika Afrika.
Ujenzi wa awamu ya kwanza unafanywa na Kampuni ya Sino Hydro kutoka China na unasimamiwa na mhandisi mshauri M/S SSI Engineers na Environmental Consultant kutoka Afrika Kusini akishirikiana na kampuni za Howard Humphrey na Nosuto Consultants za Tanzania na Netherlands Airports Consultants.
Rais Kikwete amepanda ndege hapo hapo uwanjani Tabora mara baada ya kukamilika kwa sherehe hiyo kurejea Dar es Salaam.