MKUU wa Mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe amesema kazi ya upangaji wa matumizi bora ya ardhi kwa kiasi kikubwa itapunguza na kuondoa migogoro mbalimbali ya ardhi inayotokea katika kijiji kwa kijiji, kata kwa kata au kitongoji kwa kitongoji na kusisitiza kuwa Serikali haitashindwa kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakaekwamisha kazi ya upimaji wa ardhi yenye lengo la upangaji wa matumizi bora ya ardhi.
Akizungumza na wanakijiji wa kijiji cha Dihombo, Dk. Kebwe alisema kazi hiyo itasimamiwa kikamilifu na kamati husika za ulinzi na usalama kutoka Wilayani, Kata hadi Mkoa kuhakikisha inafanikiwa. Alisema kazi hiyo inayofanywa ya upimaji wa ardhi itakuwa ndio muarobaini wa kuondoa migogoro inayojitokeza mara kwa mara ikiwemo ya Wakulima na Wafugaji katika mkoa huo.
Alisema kwa sasa wapimaji wa ardhi wanatumia vipimo vya kisasa zaidi ambavyo kwa kiasi kikubwa vipimo hivyo vitaweza kupima ardhi kwa kipindi kifupi na kila mtu kumiliki kipande cha eneo lake.
“Nakumbuka wakati wa kampeni mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alihaidi wazi kuwa kipindi cha miaka 10 kutakuwa na upimaji katika maeneo yote ya nchi kwa utaratibu wa mpango mzuri na wa kisasa,kwa miaka mitano hii vijiji takribani 7500 vitapimwa kwa kupangwa kila halmashauri 25 ambapo kwa kila mwaka vitapimwa vijiji 1500,”alisema. Alisema kuwa zoezi la upimaji linaloendelea hivi sasa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM)kwa wananchi katika kuondoa migogoro inayojitokeza.
“Kazi hii ya upimaji wa maeneo katika kuhakikisha kunampango bora wa matumizi ya ardhi ni mpango wa nchi,ambapo serikali imechangua Mkoa wa Morogoro kuwa wa Mfano katika upimaji wa ardhi ambapo utahusisha nchi nzima,”alisema Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dk. Stephen Nindi alisema ofisi yake inafanya kazi na wadau mbalimbali wa masuala ya ardhi zikiwepo wizara pamoja na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ikiwemo Shirika la Kimataifa la
Care,Shirika la Oxfam, Chama cha Wafugaji Tanzania, Chuo kikuu cha Ardhi pamoja na Tamisemi.
Dkt.Nindi alisema kwa sasa kazi ya ya upimaji inafanywa na vifaa maalum vya kisasa vijulikanavyo kwa jina la Real Time Kinematic ambavyo vinafanya kazi kwa urahisi zaidi,licha ya vifaa hivyo kwa sasa vipo viwili nanvyakukodisha. “Tunahitaji kuwa na vifaa hivi walau vitano ambavyo vitatuwezesha kupima kwa wakati na kukaimilisha zoezi hili kwa haraka na kifaa kimoja kinagharimu kiasi cha sh.milioni 80,”alisema Dk. Nindi.
Naye Mratibu wa Programu ya Ufugaji Asili kutoka Shirika la Kimataifa la Care, Marcely Madubi alisema suala la ardhi ni moja ya masuala muhimu yanayozingatiwa na shirika lao katika mikakati yao ya kimataifa. Alisema wadau
mbalimbali nchini wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika kuchangia suala hili la kuhakikisha upimaji wa ardhi unafanikiwa hususani katika kuchangia ununuzi wa vifaa vya teknolojia mpya ya upimaji (Real Time Kinematic) ili kuwezesha upimaji wa ardhi kwenda kwa haraka zaidi na kupunguza migogoro inayoendelea kujitokeza.
Picha zote na Fredy Njeje.