Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com
SERA ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000, imenukuu sehemu ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 1984. Sehemu hiyo inaeleza kwamba Tanzania ni nchi inayothamini usawa na haki za binadamu. Katiba pia inasisitiza usawa na heshima kwa binadamu wote, heshima ya kutambua na kuthamini utu wa mtu pamoja na kuhakikisha haki mbele ya sheria.
Hata hivyo wakati Katiba ya nchi na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia inasisitiza hayo bado hali ya unyanyasaji wanawake kwa vipigo nchini Tanzania inajitokeza kwa kiasi kikubwa hasa maeneo ya vijijini.
Kwa mujibu wa utafiti wa kihabari (journalistic survey) uliofanywa mwezi Aprili 2012 na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari katika mikoa 20, ikiwepo 15 ya Tanzania Bara na mitano ya Zanzibar kuhusu hali ya vitendo vya ukatili nchini. Bado suala la vipigo kwa wanawake limejitokeza kiasi kikubwa.
Ripoti ya utafiti huo inaonesha kuwepo kwa vipigo kwa wanawake karibu kila wilaya iliofanyiwa utafiti. Kimsingi hili laweza kuwa tatizo kubwa la kitaifa. Katika familia nyingi, wanawake bado wanaendelea kupigwa na wanaume, hasa waume zao au wapenzi wao.
Na kama hiyo haitoshi taarifa za utafiti zinabainisha kuwa yapo maeneo ambayo hata viongozi wa kiserikali ngazi za jamii vijijini wamekuwa wakitoa adhabu za vipigo ambazo huwaathiri zaidi wanawake. Kipigo chochote kwa mwanamke ni kibaya kwa kuwa kinamuathiri hata katika utendaji wake wa majukumu ya uzalishaji mali.
Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2000, kupitia mwongozo wa sera ya wizara hiyo zinaeleza kuwa wanawake ni wazalishaji wakubwa hasa maeneo ya vijijini. Inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya chakula huzalishwa na akinamama.
Licha ya kundi hilo muhimu kwa uzalishaji kuwa hodari wa kuzalisha lakini halina uamuzi juu ya mali ambayo linaizalisha kutokana na mazingira ya mfumo na vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vitendo vya vipigo dhidi yao.
Lakini utafiti wa kihabari katika taarifa yake unafafanua kwamba miongoni mwa sababu za wanawake kupigwa ni ulevi, “mdomo” wa akina mama, ubabe wa akinababa, fumanizi, mfumo dume, ukiukwaji wa mafunzo ya ndoa, wivu, umaskini, “mapenzi,” ndoa za mitala, ndoa za kulazimishwa na mambo mengine.
Pamoja na hayo sheria imeweka wazi dhidi ya adhabu kwa kipigo, Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 ya mwaka 2002 kifungu 240 cha kinasema kwamba mtu yeyote aliyempiga mwenzake atakuwa ametenda kosa la jinai na atahukumiwa kwenda jela kwa muda wa mwaka mmoja.
Adhabu hii itatumika katika mzingira ambayo muathirika wa kipigo hakupata madhara makubwa sana. Aidha kifungu 241 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kwa mtu yeyote aliyemdhuru mwenzake kwa kipigo na mtu huyo kupata madhara makubwa sana.
Mfano utafiti unabainisha kuwa Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, kwa mwaka 2011 pekee kesi 14 ziliripotiwa. Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mbagala (PPCM) Fatuma Katunzi, anasema kesi za vipigo zipo na kwamba mwaka 2011 zilifikishwa kesi 6, kati ya kesi hizo 2 zilitolewa hukumu ya kifungo na faini.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Msufini Kata ya Chamazi, Muharami Mlawa, anasema kesi 5 ziliripotiwa katika mtaa huo. Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Majimatitu ‘B’ Kata ya Charambe Fadhil Mpinga anasema kesi 3 za vipigo zilifikishwa kwake. Ofisa Mtendaji Mtaa wa Mianzini Jimmy Berege, anasema uongozi wa mtaa huo ulipokea kesi 6 kati ya kesi hizo tatu ziko polisi.
Neema Lalashe (46) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Uhuru Kata ya Orukasment, wilayani Simanajiro, anasema kwa sasa vitendo vya kipigo dhidi yao vinafanyika kistaarabu tofauti na miaka ya nyuma.
“Zamani mwanaume alikuwa anafunga mikono na miguu kwenye mti ndiyo unachapwa, unapigwa mpaka unapoteza fahamu lakini siku hizi kidogo hayo mambo yamepungua, kama umekosea atakuchapa lakini hufungwi tena na kamba,” anasema Lalashe.
Mwanamama huyu anaamua kuhalalisha kipigo kutokana na mazoea, na anafikia hata kuona kipigo cha nyuma kilikuwa cha kudhalilisha zaidi kuliko kinachotolewa kwa sasa. Hali hii inaonesha ni namna gani maeneo mengine vipigo vinazoeleka na hata kuhalalishwa kijamii kutokana na kukata tamaa kimsaada.
Bi. Wandoa Edward (37) mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri, Iramba mkoani Singida, anatamani kujitoa kwenye ndoa kutokana kero za kinyanyasaji anazozipata kwa mwenza wake. “Nataka kurudu nyumbani, kwani nimechoka kuishi katika ndoa yenye manyanyaso. Nyumba yangu si salama tena,” anasema Bi. Edward.
Mtendaji wa Kata ya Karatu, Paulo Lagwen anakiri kuwepo kwa vipigo kwa wanawake kutoka kwa waume zao. Anaendelea kubainisha kuwa idadi ya vipigo kwa sasa imepungua ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo nyuma.
Anasema kwa Wilayani Karatu, vipigo dhidi ya wanawake vipo, ingawa ni nadra kwa matukio haya kukuta yanaripotiwa katika vyombo vya dola. Wanaume wa Kiiraq wamestaarabika kidogo kwa utoaji vipigo kwa sasa. Idadi ya vipigo imepungua ikilinganishwa na hapo awali.
Mkoani Mbeya maeneo ya vijijini, zipo ndoa nyingi zizovunjika kutokana na kipigo kwa wanawake. Mfano kati ya watu wote 22 waliohojiwa walikiri wanaume kuwepo wanaotoa vipigo kwa wanawake. Lucia Gwamaka mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda, anasema kupigwa kwa mwanamke ni jambo la kawaida.
Kama hiyo haitoshi tatizo la vipigo linajitokeza tena wilayani Kilolo mkoani Iringa. Taarifa ya utafiti inabainisha kuwa viongozi wanapofikishwa kwenye ofisi za kijiji kwa shitaka lolote viongozi hujichukulia sheria mkononi na kuwapiga watuhumiwa.
Kwa mfano utafiti ulishuhudia wanawake wawili ambao walikuwa na ujauzito katika Kijiji cha Kidabaga kwa nyakati tofauti wakipigwa na viongozi wa kijiji hicho na hatimaye mimba walizokuwa wamebeba zikaharibika kutokana na madhara ya vipigo.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti inadaiwa kuwa viongozi waliohusika na vipigo hivyo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kidabaga, Nicolous Katandasi na Mtendaji wa kijiji hicho, Vincent Gaifalo. Taarifa inafafanua kuwa Mwenyekiti wa Kijiji, Nicolous Katandasi mnamo mwezi Mei 2011 alimchalaza viboko 16 mama Silivia Kimata, kitendo kilichosababisha mimba ya miezi mine kuharibika.
Aidha Mtendaji wa kijiji hicho, Vincent Gaifalo alimchalaza viboko 30 Seidina Kidwangise aliyefika kijijini hapo kumzika ndugu yake na kusababisha mimba yake kutoka na mama huyo kupata ulemavu wa kushindwa kusimama na kutembea.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, dakta Deogratias Manyama anathibitisha kwamba hospitali hiyo Aprili 19, 2012 ilimpokea na kumlaza Bi. Kidwangise akiwa hawezi kusimama wala kutembea na uchunguzi ulibaini alikuwa amepoteza ujauzito huku mwili wake ukiwa na majeraha.
Jambo la kushangaza wanakijiji hao walisema kuwa ingawa mtendaji wa kijiji aliyempiga mama huyo na kumsababishia madhara hayo makubwa alikuwa amefikishwa polisi, hawaamini kuwa haki itatendeka dhidi yake kutokana na kushamiri kwa rushwa hapo kijijini na kwenye vyombo vya sheria wilayani.
“Ingawa wanakijiji wa Kidabaga wamechukua hatua na kuhakikisha kuwa viongozi hao wameondoka madarakani lakini hawajafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuumiza wanawake na kuharibu ujauzito wao,” anasema mwanakijiji mmoja ambaye hakutaka jina lake kiusalama.
Akina mama wa Kimasai nao wanapigwa lakini mila zao haziruhusu kushitaki. “Hata kama ameumizwa hawezi kusema badala yake huchinjiwa kondoo na kupewa mafuta kama tiba,” anasema Lea Saitobiki, Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji akihojiwa katika utafiti huo.
Anasema hata kama utasikia amepigwa ukienda kumuuliza anakataa kata kata kuwa amepigwa. Kufuatia masuala hayo kufanywa siri, hakuna takwimu zinazoonyesha tatizo la vipigo kwa wanawake lina ukubwa gani katika kata hiyo.
“Sisi kama serikali tunashindwa kuingilia mambo ya kifamilia, huwezi kwenda kwenye nyumba ya mtu ukaanza kuuliza wewe kwa nini unampiga mke wako wakati mke mwenyewe hajawahi kuja kuripoti,” anasema Ofisa Mtendaji Kata ya Mwembe, Athumani Mkumbwa.
Kwa mantiki hiyo kuna haja sasa ya Serikali kwa kushirikiana na wadau anuai kuhakikisha inapiga vita vitendo hivi vya vipigo kwa kundi hili ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii nzima, ili kuona kwamba vipigo kwa wazalishaji mali hawa haviendelei. Hali hii itaongeza kwa kiasi kikubwa uwajibikaji kwa kundi hili katika ngazi ya familia hivyo kujikuta inachochea maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
*********************************************************************************
*Makala haya yameandaliwa na mtandao wa dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com) kwa msaada wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA)