UNFPA Yatoa Msaada ya Vifaa vya Kufundishi Vyuo vya Afya

Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini Natalia Kanem (aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kutumia simu kwa ajili ya kufundisha wakunga na wauguzi njia ya uzazi salama, waliokaa kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali) Dkt. Otilia Gowele, Msajili wa Baraza la Uuguzi Lena Mfalila na Geeta Lal kutoka makao makuu ya UNFPA

Na; Lilian Lundo – MAELEZO

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNFPA) limekabidhi simu za kufundishia huduma ya uzazi salama kwa vyuo vya Afya pamoja na taasisi zinajihusisha na masuala ya afya ya mama na mtoto ili kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito na watoto wanaozaliwa.

Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam Machi 21, 2016 baina ya shirika la UNFPA na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Akikabidhi vifaa hivyo Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini Natalia Kanem alisema wanashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuboresha elimu juu ya uzazi salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Wawakilishi kutoka Vyuo vya Afya na Taasisi zinazojihusisha na uzazi salama nchini  wakifuatilia mafunzo ya uzazi salama kwa kutumia teknolojia mpya ya simu.

Wawakilishi kutoka Vyuo vya Afya na Taasisi zinazojihusisha na uzazi salama nchini wakifuatilia mafunzo ya uzazi salama kwa kutumia teknolojia mpya ya simu.

“Dhumuni la matumizi ya simu za kufundishia uzazi salama ni kutoa elimu kwa wauguzi na wakunga walioko vijijini na maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi ili kuwasaidia kupata elimu ya uzazi salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto,” alisema Natalia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Otilia Gowele ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali alisema kuwa simu hizo zitarahisisha ufundishaji kwa wauguzi na wakunga kwani zitawawezesha kujifunza masuala yote yanayohusu uzazi salama bila kuondoka kwenye vituo vyao vya kazi.

Dkt. Gowele aliongeza kwa kusema kuwa, simu hizo zitakuwa na mafunzo ya uuguzi ambayo yako katika mitaala ya vyuo vya uuguzi na mtumiaji wa simu hiyo anaweza kuuliza swali lolote linalohusu uzazi salama akapata majibu kwa njia ya sauti, picha na maandishi.

Aidha, simu hizo zinachajiwa kwa kutumia umeme wa mwanga jua, umeme wa wakawaida na inatumia betri pia, hivyo inaweza kutumika hata maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme.

Geeta Lal kutoka Makao Makuu ya UNFPA akitoa maelekezo kwa washiriki (hawapo pichani) kuhusu mafunzo ya uzazi salama ambayo yanapatikana ndani ya simu hiyo.

Geeta Lal kutoka Makao Makuu ya UNFPA akitoa maelekezo kwa washiriki (hawapo pichani) kuhusu mafunzo ya uzazi salama ambayo yanapatikana ndani ya simu hiyo.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Afya ya Mama na Mtoto wa UNFPA Felister Bwana alisema kuwa, simu hizo zimegawiwa kama majaribio kwa baadhi ya vyuo vya Afya na na taasisi zinazojihusisha na uzazi salama, endapo teknolojia hiyo italeta mafanikio yanayotarajiwa simu hizo zitagawanywa kwa vyuo vyote vya uuguzi na hospitali nchini.

Vyuo na taasisi ambavyo vimepokea vifaa hivyo ni pamoja na Chuo cha Afya Kilosa, Bugando, Newala, Nachingwea, Bagamoyo, Geita, Kahama, Maswa, Sengerema, KCMC, Zanzibar, Ifakara pamoja na taasisi ya TAMA na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kwa mujibu ya sensa ya mwaka 2010, jumla ya vifo 454 vimekuwa vikitokea katika kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka, idadi hiyo imepungua na kufikia vifo 432 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.