UNDP Yazinduwa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu 2015

Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mh. Anthony Mavunde (katikati) akizindua rasmi Ripoti ya Maendeleo ya Watu ya mwaka 2015 (Human Development Report 2015) kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 11, 2016.

Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mh. Anthony Mavunde (katikati) akizindua rasmi Ripoti ya Maendeleo ya Watu ya mwaka 2015 (Human Development Report 2015) kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 11, 2016.

 

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Antony Mavunde ametaka kuondolewa kwa changamoto maeneo ya kazi ili kazi isaidie maendeleo ya binadamu badala ya kujikimu.

Naibu Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua ripoti ya maendeleo ya binadamu ya mwaka 2015 inayoelezea kazi kwa maendeleo ya binadamu.

Alisema kwa sasa kuna figisu kubwa katika kazi nchini hasa kutokana na waajiri wengi kugeuza kazi kama sehemu ya kujikimu kwa wafanyakazi wao kwa kutowapa stahiki husika ikiwamo mikataba ya ajira.

Alisema kazi inapokuwa ni ya kujikimu kunakuwa na migogoro mingi na kuvurugika kwa uzalishaji na kutishia maendeleo ya taasisi husika na maendeleo ya mtu binafsi.

Alisema Tanzania imefurahishwa na yaliyomo katika ripoti hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kutokana na kuzungumzia jinsi kazi zinavyoweza kusaidia upatikanaji wa maendeleo.

Alisema wakati Tanzania inaelekea kujipanga kwa uchumi wa kati, Ripoti inaonyesha ni jinsi gani kazi inaweza kuboresha maisha ya Mtanzanzania kwa kuondoa kazi na kuwapatia wananchi kazi zenye staha na zinazoweza kuwasaidia wao binafsi na hivyo kukuza uchumi na ustawi wa jamii.

Alisema amekuwa akizungumza katika maeneo mengi ya kazi na kukutana na changamoto nyingi zikiwemo za kukosekana kwa mikataba, mazingira mabaya ya kufanyakazi, ujira usiokidhi na kutaka waajiri kufuata sheria za kazi kwa kuwapatia mikataba ya kazi na pia kuhakikisha kazi zinakuwa na staha.

Awali akizungumza na wageni waalikwa katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam, alisema kwamba uzinduzi wa kitaifa ambao unafuatia uzinduzi wa kimataifa uliofanyika mwaka jana mjini Addis Ababa, Ethiopia ni faraja kubwa kwa wadau wa maendeleo nchini.

Alisema uzinduzi huo unaweka ripoti hiyo karibu zaidi na wananchi na kuahidi serikali kuifanyia kazi kutokana na umuhimu wake hasa wa kuhakikisha kazi inasaidia maendeleo ya watu.

Anthony Mavunde

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mh. Anthony Mavunde (kushoto) akibadilishana mawazo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (katikati) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida (kulia) kabla ya kuelekea kwenye uzinduzi rasmi wa ripoti ya maendeleo ya watu ya mwaka 2015 (Human Development Report 2015) uliofanyika Machi 11, 2016 jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na ESRF.

Anasema ripoti hiyo inaonesha namna ambavyo kazi inaweza kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii.

Alisema wakati Tanzania inaelekea kuwa taifa ambalo limejengeka katika msingi wa maendeleo ya watu kama ilivyokusudiwa tangu kupatikana kwa Uhuru wake 1961, Ripoti hiyo ni chanzo kizuri cha maarifa katika kufanikisha mabadiliko yanayotakiwa kufanikisha maendeleo ya watu.

Alisema kazi ni msingi wa maendeleo kwa hiyo ni vyema kuboresha mazingira ya kazi na wafanyakazi ili kuleta maendeleo kusudiwa kwa kuwa na kazi zenye staha.

Alipongeza UNDP na wadau wengine kwa kufanikisha uzinduzi huo ambao alisema umeenda sanjari na dhima ya serikali ya kutumia maarifa yote yaliyopo kusaidia maendeleo ya watu.

Ripoti hiyo ya UNDP imetazama kwa undani kuhusu kazi, mahusiano ya kazi na maendeleo ya binadamu.

Aidha imeangalia masuala ya usalama wa kazi na mahitaji ya utaalamu; masuala ya kulipwa na kutolipwa kazini, uangalizi, kujitolea ubunifu na kazi endelevu.

Pia ripoti hiyo inatoa majumuisha yanayostahili kufanywa bali mapendekezo ya utengenezaji wa sera unaotanua uzalishaji kwa kutoa fursa na kulinda wafanyakazi, ubora wa kazi, ujira stahiki, kazi yenye staha na kazi endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kimsingi Ripoti hiyo inapendekeza kuongeza faida za maendeleo ya binadamu, kupitia utendaji kazi, kwa kupendekeza mikakati ya kujenga fursa za ajira, ili kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi, na kuendeleza maeneo yaliyolengwa, ambayo yatabadilisha hali halisi ya sasa.

Aidha ainaangalia Sera zilizopendekezwa, kuhakikisha utendaji kazi bora, utendaji kazi endelevu, ambayo inachangia usawa, badala ya kujenga ukosefu wa usawa, na kazi ambayo inaheshimu haki za wafanyakazi, na kuhakikisha usalama wao.

Human Development Report 2015, Tanzania

Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akisoma taarifa kwenye uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Watu ya mwaka 2015 (Human Development Report 2015) uliofanyika jijini Dar es Salaam Machi 11, 2016 na kuratibiwa na ESRF.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kuna hatua njema kwenye maendeleo ya watu katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo lakini ipo haja ya kuangalia pengo kubwa lililopo katika fursa mbalilmbali zikiwamo za kazi.

Imeelezwa ndani ya ripoti hiyo kwamba toka mwaka 2000 nchi ziloizo kusini mwa Jangwa la Sahara zimekuwa na ukuaji wa maendeleo ya binadamu( Human Development Index -HDI) wa kazi wa kiwango cha asilimia 1.7 kati ya mwaka 2000 na 2010 : asilimia 0.9 kwa mwaka 2010 na 2014.

HDI ni kipimo kinachotathmini maendeleo ya muda mrefu ya afya na maisha marefu, elimu na maisha yenye staha.

Kwa Tanzania kumekuwepo na ongezeko la HDI la asilimia 1.18% kati ya mwaka 1985 na 2014, ikiongezeka kutoka 0.371 hadi 0.521, ikiwa ni ongezeko la asilimia 40.5 juu ya ongezeko la nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara la 0.518.

Mratibu wa Umoja wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akizungumza katika uzinduzi huo alisema kwamba ongezeko hilo si haba.

Hata hivyo aliwaambia wadau waliokuwepo kushuhudia uzinduzi huo kwamba Taifa bado linakabiliwa na changamoto nyingi zikkiwemo umaskini uliokithiri, kutanuka kwa pengo la usawa na kushindwa kuhimili matukio ya mabadiliko ya tabianchi na uchumi.

Aidha alisema kwamba :”Ripoti ya maendeleo ya binadamu ya mwaka 2015, inaonyesha kuwa, kuimarisha maendeleo ya binadamu, kupitia utendaji kazi, inahitaji sera na mikakati katika maeneo makuu matatu: kujenga fursa za ajira, kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi na kuendeleza maeneo yaliyolengwa. Hii inaongeza kasi ya kutengeneza ajira nchini Tanzania.”

Tanzania ikiwa na zaidi ya watu milioni 12 wakiishi katika umaskini na wengi wao uliokithiri changamoto kubwa kwa Tanzania, ni kutafsiri uwezo huu katika miundombinu inayoonekana, kwa kujenga mazingira mazuri, na kuongeza ujuzi wa watu wake kama ilivoainishwa katika Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu mwaka elfu mbili na kumi na tano.

Alisema changamoto zote hizo ni za kweli na zenye uhusiano na maendeleo ya binadamu na ni vyema ilivyowekwa katika Muono wa maendeleo ya Tanzania kufikia 2025 na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Katika hotuba yake ya shukurani Mkurugenzi Mkazi wa UNDP nchini, Awa Dabo, alisema kwamba taasisi yake ipo tayari kusaidia Tanzania na nchi nyingine kuwezesha kutambua uhusiano kati ya kazi na maendeleo ya binadamu katika utekelezaji wa Maendeleo endelevu (SDGs).