Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo Duniani (UNDP) limeeleza kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta za maendeleo Zanzibar yatasaidia kutekeleza malengo ya Umoja wa Mataifa (UN) ya Mpango wa ‘Kufanya Kazi Pamoja’.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo nchini Tanzania, Dk. Alberic Kacou ameyasema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu Mjini Zanzibar.
Dk. Kacou alimueleza Rais Shein kuwa UNDP inajivunia mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana chini nchini ya uongozi wa Dk. Shein na kusisitiza kuwa malengo ya UN ya Kufanya Kazi Pamoja yataleta ufanisi zaidi.
Alieleza kuwa Umoja wa Mataifa Tanzania umekuwa ukibuni njia mpya za kufanya kazi pamoja na Serikali ili kupata mafanikio makubwa kwa kuwa na kuunganisha utendaji kazi kati ya mashirika yake mbali mbali.
Kuisaidia Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kuimarisha uwezo wa Serikali katika kukuza Utawala Bora, upatikanaji wa maji na mahitaji ya msingi ya usafi wa mazingira na usafi wa mwili,elimu bora kwa wote, afya na lishe, dharura na majanga, maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kupambana na umasikini pamoja na changamoto nyenginezo.
Dk. Kacou alieleza kuwa mabadiliko ya Kufanya Kazi Pamoja yanalenga kuelekeza programu kwenye maeneo ambayo Umoja wa Mataifa unaweza kuleta matokeo mazuri kwa Tanzania nzima ikiwemo Zanzibar.
Mwakilishi huyo alieleza kuwa Shirika la UNDP linathamini sana na litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikiali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo chini ya uongozi wa Dk. Shein na kutoa pongezi zake kwa kutimiza miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar na mafanikio yaliopatikana ndani ya miaka hiyo.
Alisema kuwa hivi sasa Zanzibar hatua kubwa zimefikiwa katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemoelimu, miundombinu ya barabara, mawasiliano, maji, umeme, afya na nyenginezo.
Aidha, Dk. Kacou alieleza kuwa Mpango Mkakati wa miaka minne wa Umoja wa Mataifa, wa mwaka 2011-2015, umeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania hatua ambayo imeweza kuonesha uwazi na uwajibikaji mkubwa kati ya washirika wa maendeleo na Tanzania.
Alisema kuwa Tanzania pia, imeweka historia kwa kuwa nchi ya kwanza ulimwenguni kuibua Waraka wa Programu ya Pamoja katika ngazi ya nchi (CCPD) ambao ni sehemu ya Mpango wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDAP).
“UNDP, imemedhamiria kwa makusudi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kwani inatambua juhudi kubwa zinazochukuliwa chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuimarisha sekta za maendeleo, kiuchumi, kisiasa na kijamii,” alisema Dk. Kacou.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Shirika la UNDP kwa mashirikiano yake makubwa kati yake na Zanzibar hali ambayo imepelekea mafanikio makubwa kuweza kupatikana.
Alieleza kuwa Shirika hilo limeweza kusaidia shughuli mbali mbali za kijamii na kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA) na kueleza matarajiyo yake makubwa ya mafanikio katika Mpango huo wa ‘Kufanya Kazi Pamoja’.
Dk. Shein alisema kuwa juhudi zilizofanywa na Zanzibar kwa kuweza kuziweka pamoja afisi zote za Umoja wa Mataifa (ONE UN), kuwa kwenye jengo moja ni hatua moja wapo ambayo itasaidia kufikikia lengo la mpango wa ‘Kufanya Kazi Kwa Pamoja’.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla inatambua na inathamini juhudi za Umoja wa Mataifa na Mashirika yake kwa jinsi yanavyofanya kazi na kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na wananchi.
Akieleza juu ya mafanikio yaliopatikana kisiwani Pemba, Dk. Shein alimueleza Mwakilishi huyo kuwa haja ya kuendelea kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali katika uimarishaji wa sekta za maendeleo katika kijiji cha Micheweni Pemba.
Dk. Shein alisema kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba na kutoa pongezi kwa washirika wa maendeleo likiwemo Shirika la UNDP katika kuunga mkono juhudi hizo.