UN yapanga vikwazo dhidi ya Sudan

wanajeshi wa Sudan

Marekani imeandaa azimio ambalo limelenga kuidhinisha vikwazo dhidi ya serikali za Sudan na Sudan kusini ikiwa hazitasitisha mapigano mara moja na kurejea kwenye mazungumzo ya amani.
Azimio hilo linaunga mkono pendekezo la Umoja wa Afrika mapema wiki hii.
Muungano wa Afrika umezitaka Sudan na Sudan Kusini kutekeleza mkataba wa amani kwa muundo mpya wa AU.
Azimio hilo linazingatia sana onyo llilotolewa na Umoja wa Afrika ambapo nchi hizo zilitakiwa kuondoa vikosi vyao kwenye mipaka inayozozaniwa katika kipindi cha saa 48.
Hii ni njia moja ya kidiplomasia inayotumiwa kuzuia vita kati ya majirani hao.
Serikali ya Sudan, imelaaniwa kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Sudan kusini ikitumia ndege zake za kijeshi. Tayari Sudan kusini imeondoa wanajeshi wake kutoka eneo la Heglig ambalo walikuwa wameliteka.
Wanadiplomasia wanasema azimio hilo huenda likaungwa mkono na nchi nyingi kwa kuwa jumuiya ya kimataifa inataka sana kuepuka vita kati ya nchi hizo mbili.
China ambayo inauwezo wa kupiga kura ya turufu kuzuia vikwazo hivyo inaonyesha dalili kuunga mkono azimio hilo.
Hata hivyo huenda hilo likabadilika wakati vikwazo hivyo vitakavyo pendekezwa vitaorodheshwa na Marekani.

-BBC