UN Yaizuia Iran Kushiriki Mkutano wa Kusaka Aman Syria

UN Yaizuia Iran Kushiriki Mkutano wa Kusaka Aman Syria

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon amesitisha mwaliko wa kutaka nchi ya Iran kushiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu kati ya pande zinazozozana nchini Syria. UN imefikia uamuzi huo baada ya Iran kutupilia mbali mashariti yaliyokuwa yakiambatanishwa na mwaliko huo wa kushiriki mazungumzo.

Msemaji wa UN, Martin Nesirky alisema Ban Ki-moon ameubatilisha mwaliko wa Iran baada ya nchi hiyo kukiuka yale waliyokubaliana, ikiwemo nchi hiyo kuunga mkono maazimio ya mkutano wa Geneva.

“Katibu Mkuu amehuzunishwa sana na tangazo lililotolewa na Iran, ambalo ni kinyume kabisa na ahadi iliyokuwa imetolewa, na anaendelea kuitolea wito nchi hiyo kuunga mkono maazimio ya mkutano wa Geneva,” alisema Nesirky.

Mwaliko huo uliotolewa ghafla juzi jioni haukudumu hata kwa saa 24, na ulikuwa umesababisha mtafaruku mkubwa, huku upinzani nchini Syria ukitishia kutohudhuria kabisa mkutano wa kesho iwapo Iran ambayo ni mshirika mkubwa wa rais Bashar al-Assad ingeshiriki kwenye meza ya mazungumzo.

Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif alikuwa amemhakikishia Ban Ki-moon kwamba anaelewa vilivyo, na anaunga mkono lengo la mazungumzo ya amani ambalo ni kuunda serikali ya mpito.

Lakini kabla ya kubatilishwa kwa mwaliko huo kwa Iran, balozi wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa, Mohammad Khazaee alikaririwa akitoa msimamo wa serikali yake, kwamba ikiwa kushiriki kwake katika mazungumzo kunajumuishwa na masharti ya kukubali maazimio ya mkutano wa kwanza wa Geneva, basi haitakwenda katika mkutano wa pili.

Umoja wa Mataifa umesema Ban alifanya mashauriano na Marekani na Urusi kabla ya kufuta mwaliko kwa Iran. Marekani imesema inazo taarifa kutoka ndani ya serikali ya mjini Damascus, kwamba serikali hiyo inataka suluhisho la amani kwa mgogoro unaoendelea nchini humo.

Ingawa mkutano wa Montreux ambao pia umepachikwa jina la Geneva II unaanza kesho, wajumbe wa serikali ya Syria na wa upinzani wataanza kuzungumza Ijumaa. Bado vipo vizingiti vikubwa kwa mazungumzo hayo, ambavyo vimedhihirishwa na mpasuko wa ndani kwa upande wa waasi, msimamo mkali wa rais Bashar al-Assad, na kuendelea kwa ghasia ambazo zinavuka mpaka na kuingia katika nchi jirani.

Urusi ambayo ni mshirika wa serikali ya Syria na mmoja wa waandaaji wa mkutano wa Geneva, imesema litakuwa kosa kubwa kutoishirikisha Iran katika mkutano huo. Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow muda mfupi uliopita, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema bila Iran mkutano wa kesho hautakuwa na chochote zaidi ya utaratibu wa kiitifaki.

Iran nayo imesema ina mashaka juu ya mafanikio ya mkutano huo. Muungano mkuu wa upinzani dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad umesema utakwenda kwenye mkutano huo utakaofanyika mjini Montreux, lakini kundi jingine kubwa lijulikanalo kama Baraza la Kiataifa la Syria limejitenga na mazungumzo hayo, likishikilia msimamo wake wa kutoshiriki mazungumzo yoyote hadi pale rais Assad atakapokuwa ameondoka madarakani.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria ambalo lina makao yake nchini Uingereza, takribani watu 130,000 wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria ambavyo vilizuka tangu mwaka 2011.

-DW