UMOJA wa Mataifa (UN) umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwa uamuzi wake wa kutoa uraia wa Tanzania kwa waliokuwa wakimbizi 162,156 wa Burundi. Pongezi hizo za UN zimetolewa Oktoba 16, 2014, na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Eneo la Maziwa Makuu, Balozi Said Djinnit wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika Ikulu Ndogo, mjini Dodoma.
Balozi Djinnit amesema kuwa uamuzi huo wa Rais Kikwete kutoa uraia kwa mamia ya wakimbizi hao wa Burundi unathibisha na kudumisha tunu za kihistoria ya ukarimu zaTanzania ambazo zimethibitisha mara kwa mara tokea Uhuru mwaka 1961.
Balozi Djinnit amemwambia Rais Kikwete: “Nikiwa Mwafrika na Mwakilishi wa Umoja wa Taifa ni jambo la kufurahisha na kutia matumaini sana kuwa Tanzania inaendelea kuwa mfano katika kupokea, kuwatunza na hatimaye kutoa uraia kwa wakimbizi. Ni mwendelezo wa tunu za kudumu za Tanzania.”
Ameongeza Balozi Djinnit, “Uamuzi wako huo Mheshimiwa Rais ambao ni uamuzi wa Tanzania na unakwenda sambamba na tunu za nchi hii ya Tanzania na pia tunu za Umoja wa Afrika (AU).”
Balozi Djinnit pia amempogeza Rais Kikwete na uongozi wote wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiunga na Jeshi la Umoja wa Mataifa la Force Intervention Brigade (FIB) la Kulinda Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Ushahidi uko wazi kuwa Kikosi cha Tanzania ndicho chenye nguvu kubwa zaidi na mchango mkubwa zaidi katika FIB na tunapongeza na kukushukuru kwa kukubali kutoa askari wa nchi hii kuingia katika FIB. Vijana wanafanya kazi kubwa na nzuri sana,”. Balozi Djinnit amemwambia Rais Kikwete.
Aidha, Balozi Djinnit amempongeza Rais Kikwete na Tanzania kwa kukubali kusuluhisha pande zinazopingana ndani ya chama tawala cha Sudan Kusini cha Sudanese People’s Liberation Movement (SPLM). Jitihada hizo za usuluhishi ambazo zinafanywa kichama kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeanza mjini Arusha baada ya maombi ya chama chenyewe cha SPLM yaliyowasilishwa kwa Rais Kikwete na uongozi wa chama hicho.
Rais Kikwete amemwambia Balozi Djinnit kuwa Tanzania imeamua kutoa uraia kwa waliokuwa wakimbizi wa Burundi kwa sababu wametimiza masharti ya kuweza kuwa raia wa Tanzania, ukiwemo ukweli kuwa wakimbizi hao wamekuwa wameishi Tanzania kwa miaka 42.
Wakati wa utoaji wa Hati za Uraia kwa raia hao wapya wa Tanzania katika sherehe iliyofanyika mjini Tabora juzi Jumanne, Oktoba 14, 2014, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), Mheshimiwa Joyce Mends-Cole alisema kuwa uamuzi huo wa Tanzania unaifanya Tanzania kuweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza duniani kutoa uraia kwa kundi kubwa zaidi la wakimbizi na kwa wakati mmoja.