Na Mwandishi Maalumu, New York, Marekani
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki Moon amesifu na kupongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wa kuundwa upya kwa Katiba ya Tanzania.
Aidha, Ban Ki Moon amepongeza hatua ya amani na utulivu uliofikiwa katika Zanzibar kufuatia maridhiano na makubaliano ya kisiasa Visiwani humo.
“Mheshimiwa Rais nakupongeza sana kwa uamuzi wako sahihi na wa busara wa kisiasa wa kuangalia upya Katiba ya sasa ya nchi hiyo kwa nia ya kutungwa kwa Katiba mpya kwa sababu hatua hiyo dhahiri itaendeleza utulivu ambao umedumu Tanzania kwa miongo mingi,” Ban Ki Moon amesema.
Ban Ki Moon ameyasema hayo Oktoba 2, 2012, wakati alipompokea Rais Kikwete kwa mazungumzo ofisini kwake kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete ambaye yuko New York, Marekani, kwa ziara ya siku mbili amekutana na Ban Ki Moon ikiwa ni shughuli yake ya kwanza rasmi tokea alipowasili mjini humo Oktoba Mosi, 2012.
Ban Ki Moon amemwambia Rais Kikwete kuwa sasa Tanzania na eneo lote la Afrika Mashariki linanufaika na uamuzi mwingine wa busara wa kisiasa wa kutafuta na kupata maridhiano katika Zanzibar. Katibu Mkuu huyo wa UN amesifu jitihada zinazofanywa na viongozi wa nchi wa eneo la Maziwa Makuu katika kuleta amani Mashariki mwa Congo (DRC).
“Niliitisha mkutano wa viongozi wa eneo hilo Septemba 27, mwaka huu, walihudhuria viongozi wengi akiwamo Rais Joseph Kabila wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda, na kuwaeleza kuwa Umoja wa Mataifa unafuatilia kwa makini matukio ya eneo hilo na kuwajulisha kuwa kama wanahitaji msaada wowote wa UN basi sisi tuko tayari,” amesema Ban Ki Moon.
Katibu Mkuu huyo pia amemwomba Rais Kikwete kusaidia maendeleo ya kisiasa katika Zimbabwe kufuatia kuchaguliwa kwa Rais kuwa mwenyekiti wa Chombo Maalum cha Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu Siasa, Ulinzi na Usalama.
“Kwa nafasi yako kama Mwenyekiti wa Chombo Maalum cha SADC ni dhahiri kuwa unaweza kuchangia sana maendeleo ya kisiasa ya Zimbabwe,” amemwambia Rais Kikwete ambaye amekubaliana na Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Rais Kikwete amemweleza Katibu Mkuu huyo kuwa uamuzi wa kuunda Katiba mpya unalenga kuwa na Katiba ambayo itaiongoza Tanzania kwa miaka 50 ijayo. “Baada ya kutumia Katiba yetu nzuri kwa miaka 50 iliyopita, tukaamua kuwa pengine ni vyema kuunda Katiba ambayo itatupeleka kwa miaka mingine 50 ijayo. Naamini hili litatusaidia.”