Umoja wa Kiarabu waunga mkono vikwazo Libya

Gaddafi

UMOJA wa Nchi za Kiarabu umeunga mkono wazo la kuzuia ndege kuruka katika anga ya Libya, huku waasi wakiendelea kufurushwa kutoka miji waliyokuwa wakiishikilia.

Mkutano maalumu uliofanyika mjini hapa umelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kuweka sera hiyo hadi mgogoro wa sasa utakapomalizika.

Uingereza na Ufaransa ziliunga mkono wazo hilo lakini hazikuungwa mkono vya kutosha na Umoja wa Ulaya (EU) au Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi (Nato).

Majeshi ya waasi ya Libya yamezidi kupata pigo ikiwamo kupoteza mji muhimu kwa mafuta wa Ras Lanuf.
Ripoti zinasema kwamba majeshi ya mstali wa mbele ya waasi yamesukumwa nyuma zaidi kuelekea mji wa Ujala.

Aidha ripoti nyingine zinasema waasi walielekea kuupoteza pia mji wa Brega jana kufuatia mapigano makali.

Umoja wa Nchi za Kiarabu ulipiga kura kuunga mkono amri ya kutoruka katika anga ya Libya, uamuzi ambao ulipingwa na nchi mbili tu Syria na Algeria, ripoti kutoka mkutano huo wa Cairo zilisema.

Awali Nato ilisema kwamba itaunga mkono wazo hilo iwapo tu eneo husika litaunga mkono.

Marekani imeukaribisha uamuzi huo wa Umoja wa Kiarabu, ikisema utaongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Kanali Muammar Gaddafi na kuwaunga mkono watu wa Libya