MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeshusha bei ya umeme kwa wateja wote Wajumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakitembelea ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme uliopo mkoani Singida wenye KV 400 kutoka Kenya. Mtambo huo utasambaza umeme katika mikoa ya Singida, Iringa na Shinyanga. Picha ya Makataba
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeshusha bei ya umeme kwa wateja wote nchini kuanzia jana na sasa Sh5,000 inaweza kununua uniti 14 badala ya kiwango hicho kutumika kwa malipo ya huduma.
Kwa bei hiyo mpya, wateja wa kawaida ambao walikuwa wakinunua uniti 27 za umeme kwa Sh10,000, sasa watapata uniti 54 baada ya malipo ya huduma (service charge) kuondolewa huku bei ya umeme ikishuka. Ewura ilitangaza punguzo hilo jana, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya kupokea maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Februari 24 ya kutaka mabadiliko ya kupunguza bei kwa miaka miwili kuanzia Aprili Mosi.
“Maamuzi ya marekebisho ya bei ya umeme kwa mwaka 2017 yameahirishwa mpaka Tanesco itakapowasilisha upya maombi hayo (ya kupunguza) kabla ya Agosti 31 mwaka huu,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi jana.
Mkurugenzi huyo alitangaza mabadiliko ya bei kwa makundi yote ya wateja, ambayo ni watumiaji wadogo wa majumbani, migahawani, viwanda vidogo na vikubwa pamoja na wasambazaji. Ngamlagosi alisema pamoja na mabadilko hayo ya bei, mamlaka yake imeondoa tozo za maombi ya kuunganishiwa umeme na tozo za mwezi maarufu kama service charges.
Alisema wateja wa kundi D1 ambao wanaotumia chini ya uniti 75 kwa mwezi, watalipa Sh100 kwa kila uniti moja na wakitaka zaidi ya uniti hizo watalazimika kulipa Sh350 kwa kila uniti itakayozidi. D1 ni wateja wa nyumbani ambao umeme wao unatolewa katika msongo mdogo wa njia moja ya volteji 230. Mwandishi wetu Julieth Kulangwa, ambaye anatumia taa nne, friji, pasi na televisheni, alipata uniti 14 aliponunua umeme wa Sh5,000 jana kuthibitisha punguzo hilo.
“Kwa kawaida nilikuwa siwezi kununua umeme kwa Sh5,000 kama sijalipa service charge ya mwezi huo ambayo ilikuwa Sh5,500,” alisema Kulangwa.
“Umeme ulikuwa headache (unaumiza kichwa). Sasa naona kama nimetua mzigo fulani. Naweza kutumia jiko langu la umeme bila ya wasiwasi, kutengeneza juisi. Mzigo umepungua kwa kweli.”
Kwa mujibu wa Ngamlagosi, kundi la pili ni T1 ambalo ni la wateja wenye matumizi ya kawaida ya nyumbani, biashara na viwanda vidogo, taa za barabarani na mabango ambao wanaunganishwa kwenye msongo mdogo kwenye njia moja yenye volteji 230 na njia tatu ya volteji 400. Alisema wateja hao walikuwa wanatozwa Sh298 na sasa watatakiwa kulipa Sh292, huku wakiondolewa malipo ya huduma ya Sh6,000.
Tofauti na makundi mengine, T2 ambao ni watumiaji wote waliounganishwa kwenye njia tatu za volteji 400 na ambao matumizi yao yanazidi uniti 7,500 wakijumuisha viwanda vya kati, migahawa, kumbi za burudani na vyuo, watalipia Sh195 kutoka Sh200 ya sasa huku wakiendelea kutozwa ‘service charge’ ya Sh14,233 kwa kila mwezi.
Watumiaji wa juu zaidi, hasa wa viwandani na wazalishaji wakubwa waliounganishwa kwenye msongo wa kati wa ambao wanawekwa kwenye kundi T3-MV, nao pia wataendelea kulipia ‘service charge’ ya Sh16,769 huku wakipata nafuu ya Sh2 kwenye kila uniti wanayotumia.
Kwao, bei imepungua kutoka Sh159 mpaka Sh157.
Kundi la mwisho ni T3-HV ambalo lina wateja waliounganishwa kwenye msongo mkubwa likiwamo Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) pamoja na kampuni ya uchimbaji madini ya Bulyanhulu na Twiga Cement, watatakiwa kulipia Sh152 kwa kila uniti, ikiwa ni punguzo la Sh6 ikilinganishwa na bei iliyopo.
Ewura pia imeagiza kuwa mteja asiyehitaji nguzo na ambaye yupo ndani ya mita 30, alipie Sh272,000 kwa waliopo mjini na Sh150,000 kwa vijijini.
Wanaohitaji nguzo moja au waliomo ndani ya mita 70 kutoka kwenye chanzo, watalazimika kulipia Sh436,964 kwa mjini na Sh286,220 kwa maeneo ya vijijini huku wale waliopo ndani ya mita 120 na anaohitaji nguzo mbili wakilipia Sh590,398 kwa mjini na Sh 385,300 kwa vijijini.
Kwa wale watakaounganishwa kwenye njia tatu; ndani ya mita 30 watalipia Sh772,893 wakati wale wa ndani ya mita 70 watapaswa kulipa Sh1,058,801 huku waliopo ndani ya mita 120 wakilipia Sh1,389,115.
Ikiwa ni sharti ambalo litatakiwa kuzingatiwa kabla ya kutoa huduma husika, Ngamlagosi alisisitiza: “Ni lazima wateja wote wafungiwe luku ili kurahisisha usomaji wa matumizi yao. Kwa waliokatiwa watalazaimika kulipa Sh7,000 ili kurejesha huduma. Wale watakaochezea mfumo wa mita, kanuni za huduma za ugavi wa umeme zitafuatwa.”
Mabadiliko hayo yametangazwa muda mfupi baada ya kukamilika kwa mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I. Punguzo hilo la bei ya umeme limeungwa mkono na wananchi waliozungumza na gazeti hili. Profesa wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Lettice Rutashobya alisema hizi ni habari njema kwa wapenda maendeleo wote nchini, mjini na vijijini.
“Umeme ni msingi wa biashara. Zipo fursa nyingi ambazo watu wa vijijini walikuwa hawazitumii kwa kukosa umeme, lakini hii inatoa matumaini.
Uhaba wa ajira utapungua na hata malalamiko kutoka kwa wananchi pia,” alisema mwanazuoni huyo na kueleza kuwa kwa mwendo huu, Tanzania ya viwanda itapatikana.
“Ni furaha ya wengi,” mwanaharakati na mchumi wa taasisi ya Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema.
Alisema sasa anaiona “Tanzania ya ahadi” na kuongeza kuwa punguzo hilo litaongeza ushindani miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa na pia kushusha gharama za maisha kwa ujumla.
“Wanachotakiwa kufanya Tanesco ni kuhakikisha umeme haukatiki mara kwa mara kwa kuwa suala hili huwaumiza sana wananchi na viwanda vidogo pia ambao hupata hasara kubwa kulingana na mitaji yao,” alisema Profesa Wangwe.
Akiipongeza Serikali kwa kujali mahitaji ya wananchi, Hellen Julius, mkazi wa Kigamboni jijini hapa, alisema kushuka kwa gharama za umeme kutapunguza migogoro kwenye nyumba za kupanga.
“Kulikuwa na shida kwenye kulipa bili ya umeme. Baadhi ya wapangaji walikuwa hawaonekani zinapofika zamu zao za kuchangia kutokana na bei kubwa iliyokuwapo. Nadhani punguzo hili litaongeza maelewano baina ya wapangaji ambao walikuwa wanaonana kwa nadra,” alisema Hellen.
CHANZO; Gazeti Mwananchi